NINI KIMEMKUTA NABY CAMARA SIMBA…..HUU HAPA UKWELI USIOSEMWA…
KWA mara ya kwanza, Septemba 10, 2025 mashabiki wa Simba na wadau wa soka nchini, walipomshuhudia Naby Camara katika tamasha la timu hiyo akiupiga mwingi dhidi ya Gor Mahia, walitambua kuwa ni mali, wakiamini anaweza kuwa sehemu muhimu ya kikosi hicho, lakini ghafla upepo umegeuka.
Ni miezi saba sasa tangu nyota huyo raia wa Guinea alipowakosha mashabiki wa Simba kwenye tamasha hilo wakati huo Wekundu wa Msimbazi wakiwa chini ya Kocha Fadlu Davids, aliyevutiwa naye na kupitisha usajili wake wakati wa maandalizi ya msimu huu ambayo timu hiyo ilifanya Misri.
Ndani ya miezi saba kila kitu kimebadilika kwa Camara kutoka kuwa mchezaji mwenye uwezo wa kutumika zaidi ya nafasi moja uwanjani ikiwemo beki wa kushoto, beki wa kati, kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji, sasa amekuwa akiishia jukwaani, haonekani kuwa na nafasi chini ya Steve Barker ambaye alirithi mikoba ya Dimitar Pantev, Desemba 19, 2025.
Licha ya kuwa na uwezo wa kutumika katika maeneo hayo, Barker ameonyesha kupendelea kuwatumia Nickson Kibabage ikiwa ni ingizo la dirisha dogo la usajili la Januari 2026, huku Anthony Mligo akionekana kushindwa kuvaa viatu vya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyeondoka ulipomalizika msimu wa 2024-2025.
Nini kimemkuta Camara? Haonekana kuwa hata chaguo la pili katika nafasi zote mbili, ikiwa ni pamoja na eneo la kiungo cha chini ambalo Barker amependelewa kuwatumia Yusuph Kagoma, Alassane Kante na wakati mwingine amekuwa akicheza Neo Maema.
Mara ya mwisho kwa Camara kuichezea Simba ilikuwa Februari 11, 2026 wakati timu hiyo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC, aliingia dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Kibabage.
Tangu hapo, nyota huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto ameishia benchi (mchezaji wa akiba) katika mechi saba ambazo ni dhidi ya dhidi ya TRA United, Coastal Union, TRA United, Pamba Jiji, Singida Black Stars, Yanga (mzunguko wa kwanza) na Tanzania Prisons.
Kwa upande mwingine, alikuwa nje ya kikosi, yani hakuwa hata katika machaguo ya wachezaji wa akiba katika mechi saba ikiwemo tano mfululizo zilizopita dhidi ya Tanzania Prisons, JKT Tanzania, Yanga, Namungo na Fountain Gate, huku nyingine ikiwa dhidi ya Azam na Dodoma Jiji.
Kwa sasa siku za Camara ndani ya Simba zinahesabika, inaelezwa kuwa hayupo kwenye mipango ya Barker kutokana na sababu mbili tofauti ambazo zimeelezwa na chanzo cha ndani jambo linaloathiri nafasi ya kutumika kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Barker anahitaji kuwa na beki wa pembeni mwenye kasi na ufanisi mkubwa katika kushambulia kama ilivyo kwa Kibabage, Mligo anaonekana kuwa na nafasi ya kukua, tofauti na Camara ambaye ni mchezaji wa kigeni ana jukumu la kuonyesha vile anaweza kuwa msaada, kushindwa kwake kutimiza jukumu hilo kunalifanya benchi la ufundi la Simba kufikiria mchezaji mwingine ambaye anaweza kuwa na mchango zaidi.
“Sio kwamba Camara ni mchezaji mbaya, hapana, lakini nafasi ikiwa finyu kwake kuna wachezaji wanafanya vizuri zaidi kwenye nafasi ambazo pengine angetumika,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho ambacho ni sehemu ya benchi la ufundi la Simba, kiliongeza kwa kusema, Camara ni mzuri endapo Simba itaamua kumtumia kama beki wa kushoto ambaye atatakiwa kucheza zaidi eneo la kati, hivyo anaweza kuongeza idadi ya viungo kitu ambacho ni tofauti kabisa na mbinu za Barker.
Hata hivyo, chanzo hicho kilisema kwa upande wa eneo la kati, Camara ni mchezeshaji mzuri, lakini sio mchezaji ambaye anaweza kutumika kucheza katika eneo kubwa la uwanja kwa ufanisi uleule kama ilivyo kwa Kante na Kagoma.
Inaelezwa kuwa, Simba ipo tayari kuachana naye mwisho wa msimu huu ili kutumia nafasi hiyo kushusha mashine nyingine ambayo inaweza kuongeza nguvu zaidi kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Kombe la Muungano 2026.
Zaidi ya hayo, mwenendo wa kikosi cha Simba katika kipindi cha hivi karibuni umeonyesha kuwa ushindani wa nafasi umeongezeka kwa kiasi kikubwa, jambo linalowalazimu wachezaji kuonyesha ubora wa juu kila wanapopata nafasi.
Hali hii imekuwa ngumu zaidi kwa Camara ambaye hajapata mwendelezo wa kucheza unaoweza kumsaidia kurejesha kiwango chake na kujiamini zaidi uwanjani.
Pia mabadiliko ya mbinu kutoka kwa benchi la ufundi yameonekana kuathiri aina ya wachezaji wanaopewa kipaumbele. Mfumo unaotumiwa sasa unahitaji wachezaji wenye kasi, nguvu na uwezo wa kuchangia moja kwa moja katika mashambulizi, hasa kwa mabeki wa pembeni. Hii imeifanya nafasi ya Camara kupungua kutokana na kutokidhi mahitaji hayo ya kiufundi.
Mshambuliaji wa zamani wa Stand United na Mbeya City, Abasarim Chidiebele, alisema ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho ndiyo unaomfanya Camara kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
“Simba ya sasa ina ushindani mkubwa sana hasa baada ya usajili ambao walifanya Januari, kwa hiyo ukishuka kiwango kidogo unakaa nje, unakumbuka kilichotokea kwa Mpanzu (Elie). Camara ni mchezaji mzuri lakini anaonekana kushindwa kuendana na kocha, anatakiwa kubadilika na kupigania nafasi,” alisema Chidiebele.
Kwa upande wake, Amri Kiemba ambaye aliwahi kuzichezea Simba, Yanga na Azam, alisema tatizo kubwa kwa Camara ni kutokupata mwendelezo wa kucheza jambo lililoathiri kujiamini kwake.
“Ubaya ni kwamba hizi klabu kubwa hasa kwa mchezaji wa kigeni kama ukishindwa kuwa na nafasi ni rahisi kukuacha na kutumia nafasi hiyo kuleta mchezaji mwingine,” alisema.