Habari za michezo

VITA YA TIKETI NUSU FAINALI YANGA SC WAVAMIA KAMBI ZA JESHI

Vardo May 16, 2026 7:42 pm

MABINGWA watetezi wa kombe la ashirikishoa la CRDB Yanga SC leo Mei 16, 2026 wanashuka dimbani kuvaana na JKT Tanzania katika mchezo wa robo fainali unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Timu hizo mbili zitapambana kusaka tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Meja Jeneral Isamuhyo kuanzia saa 12:30 jioni, huku kila upande ukiingia ukiwa na dhamira moja tu ya kupata ushindi.

Mshindi wa mchezo huo atafuzu moja kwa moja hatua inayofuata, wakati timu itakayopoteza itaaga rasmi mashindano hayo hadi msimu ujao wa mwaka 2027.

Kocha Mkuu wa Yanga SC, Abdihamid Moalin, amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa ajili ya pambano hilo muhimu, akisisitiza kuwa lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele kwenye hatua ya nusu fainali.

Moalin amesema anatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini anaamini maandalizi waliyoifanya yatawapa nafasi nzuri ya kufanikisha malengo yao ndani ya dakika 90.

“Tunatambua mchezo utakuwa mgumu, tumefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo na malengo ni kuona kwamba tunasonga mbele hatua inayofuata,” amesema Moalin.

Pambano hilo pia linaongeza uzito kutokana na historia ya timu hizo kwenye mashindano hayo, ambapo Yanga SC wanaingia kama mabingwa watetezi, huku JKT Tanzania wakikumbukwa kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali mwaka 2025.

Leo wanapata nafasi nyingine ya kupigania ndoto zao mbele ya mashabiki wao katika mazingira ya kambi za jeshi.

CHAMA SASA GARI IMEWAKA KUTOKA KITANDANI HADI GYM, NANGUA AREJEA KWA KASI