Habari za michezo
KUTOKA KITANDANI HADI GYM, NANGUA AREJEA KWA KASI
Vardo
May 16, 2026
7:47 pm
BEKI wa Simba SC, Wilson Nangua, ameanza rasmi mazoezi binafsi ya GYM ikiwa ni hatua muhimu katika safari yake ya kurejea uwanjani baada ya kuuguza majeraha makubwa ya kifundo cha mguu yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji nchini South Africa.
Nangua alipata majeraha hayo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Espérance Sportive de Tunis mwezi Februari, hali iliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu na kuwavunja moyo mashabiki wengi wa Msimbazi waliokuwa wameanza kuvutiwa na uwezo wake mkubwa ndani ya kikosi hicho.
Hata hivyo, taarifa za sasa zinaonyesha kuwa beki huyo anaendelea vizuri kiafya na tayari ameanza programu za kurejesha utimamu wa mwili. Hatua yake ya kuanza mazoezi ya GYM inaonekana kuwa ishara nzuri ya maendeleo, ikionyesha kuwa safari yake ya kurejea dimbani inaanza kuingia kwenye hatua chanya.
Kutoka kutembea kwa tahadhari hadi kuanza mazoezi mepesi ya nguvu mwilini, Nangua anaonyesha dalili za kurejea taratibu katika ubora wake. Wadau wengi wa soka wanaamini kuwa kurejea kwake kutakuwa habari njema kwa Simba kuelekea msimu ujao.
Kabla ya kuumia, Nangua alikuwa ameanza kujijengea nafasi ndani ya kikosi cha Simba kutokana na utulivu wake akiwa na mpira, uimara katika mipambano pamoja na ujasiri mkubwa licha ya umri wake mdogo. Wengi walimuona kama mmoja wa mabeki wenye uwezo wa kuwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya timu hiyo kwa miaka ijayo.
Kwa sasa, safu ya ulinzi ya Simba ina mchanganyiko wa uzoefu na vipaji vya vijana. Wapo mabeki wenye uzoefu mkubwa kama Rushine De Reuck na Ismael Toure, huku Abdulrazack Hamza akiendelea kuonyesha kiwango kizuri licha ya kusumbuliwa mara kwa mara na majeraha.
Aidha, vijana kama Vedastus Masinde na Yahya Mbegu wameendelea kuonyesha uwezo mkubwa kila wanapopewa nafasi.
Kurejea kwa Nangua kutakuwa nyongeza muhimu kwa Simba, hasa wakati timu hiyo ikijiandaa kwa changamoto za msimu ujao na mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa