Habari za michezo

MANGUNGU AAMINI SIMBA BADO INA NAFASI YA KUTWAA TAJI

Vardo May 16, 2026 8:03 pm

MWENYEKITI wa klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu, amesema bado wana imani kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu huku akisisitiza kuwa kikosi hicho kitaendelea kupambana hadi mwisho wa msimu kuhakikisha kinafikia malengo waliyojiwekea.

Mangungu amesema ligi imeingia katika hatua muhimu yenye ushindani mkubwa, ambapo kila timu inapambana kuhakikisha inamaliza msimu katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi.

Ameeleza kuwa kwa sasa wamebakiza takribani mechi nane au tisa, hali inayomaanisha bado kuna pointi nyingi za kuwania ambazo zinaweza kubadilisha kabisa mwenendo wa mbio za ubingwa.

Kwa mujibu wa Mangungu, hali hiyo inaifanya Simba SC kuendelea kuwa na matumaini makubwa ya kutwaa taji hilo, hasa kutokana na kiwango kizuri ambacho timu imekuwa ikikionesha katika michezo ya hivi karibuni.

“Bado tunaendelea kupambana na timu yetu inaendelea kufanya vizuri. Malengo yetu makubwa ni kutwaa ubingwa. Tunapozungumzia mechi nane, maana yake ni pointi 24 ambazo bado zipo mezani,” amesema Mangungu.

Amesema uongozi wa klabu kwa kushirikiana na benchi la ufundi unaendelea kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya michezo iliyobaki ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika hali bora ya ushindani kila wanapoingia uwanjani.

Mangungu ameongeza kuwa wanaamini kwa umoja, nidhamu na kujituma kwa wachezaji pamoja na sapoti kutoka kwa mashabiki, Simba SC inaweza kumaliza msimu kwa mafanikio na kufikia ndoto ya kutwaa ubingwa wa ligi.

SIMBA YABEBA MORALI KIGOMA, SASA YAWINDA TIKETI BARKER AFUNGUKA HATMA YA BAJABER SIMBA SC