Habari za michezo
SIMBA YABEBA MORALI KIGOMA, SASA YAWINDA TIKETI
Vardo
May 16, 2026
7:59 pm
KIUNGO wa Simba SC, Neo Maema, amesema kikosi hicho kimehamishia nguvu zote katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United baada ya kukamilisha kazi yao ya kusaka alama tatu mkoani Kigoma.
Simba imerejea leo Mei 16, 2026 kutoka Kigoma ilikocheza dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanikiwa kuondoka na ushindi muhimu uliowaongezea morali kwenye mbio zao za msimu huu.
Mara baada ya kurejea jijini, kikosi hicho kiliingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TRA United, utakaochezwa katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
Maema amesema ndani ya kikosi hicho kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo huo kutokana na kuwa wa mtoano, hali inayowalazimu kuingia uwanjani kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha wanapata ushindi.
Kiungo huyo ameeleza kuwa wanaiheshimu TRA United kutokana na ushindani waliokutana nao katika michezo yao miwili iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo linalowafanya waamini hawatakutana na mchezo mwepesi.
“Hii ni mechi ya mtoano, anayefungwa anatoka, hivyo hatutakuwa tayari kupoteza. Malengo ya klabu pamoja na wachezaji ni kuhakikisha tunatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho,” amesema Maema.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa baada ya ushindi walioupata Kigoma, huku benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo wakitarajia kuona kikosi hicho kikiendelea na mwendo wake mzuri katika mashindano ya ndani msimu huu.