Habari za michezo
BARKER AFUNGUKA HATMA YA BAJABER SIMBA SC
Vardo
May 16, 2026
8:07 pm
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Simba SC, Steve Barker, amesema bado ana matumaini makubwa ya kuendelea kumtumia kiungo Mohamed Bajaber ndani ya kikosi hicho msimu ujao, licha ya changamoto ya majeraha ambayo yamekuwa yakimkabili nyota huyo tangu kuwasili kwake klabuni hapo.
Bajaber, raia wa Kenya, amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kupata majeraha yaliyosababisha hata jina lake kuondolewa kwenye usajili wa mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hali iliyozua wasiwasi kuhusu hatma yake ndani ya kikosi cha Simba.
Hata hivyo, kiungo huyo alirejea tena dimbani mwezi Aprili mwaka huu aliposhiriki Kombe la Muungano lililofanyika visiwani Zanzibar, hatua iliyotoa mwanga mpya kuhusu maendeleo yake ya kiafya na utimamu wake wa mwili.
Katika michuano hiyo, Bajaber alionyesha kiwango kizuri kilichosaidia Simba kutwaa ubingwa, huku akipata nafasi ya kucheza baadhi ya michezo muhimu ikiwemo fainali dhidi ya Yanga SC, jambo lililoashiria dalili za kurejea kwenye ubora wake wa kawaida.
Barker amesema kurejea kwa mchezaji huyo kumempa matumaini mapya ndani ya benchi la ufundi, ingawa bado wanaendelea kumfuatilia kwa karibu ili kuhakikisha anakuwa imara kiafya kabla ya kupewa majukumu makubwa zaidi msimu ujao.
Akizungumzia hatma ya kiungo huyo, Barker alisema anatamani kumuona Bajaber akiendelea kuitumikia Simba kwa muda mrefu kutokana na ubora na uwezo wake mkubwa wa kiufundi akiwa uwanjani.
“Bajaber ni mchezaji mzuri sana na hilo linafahamika. Nataka kumuona akiendelea kuitumikia Simba msimu ujao, lakini jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha anakuwa imara kiafya ili tuepuke tena changamoto za majeraha,” amesema Barker.