Habari za michezo
YANGA YAWEKA WAZI, HATUOGOPI AZAM WALA MASHUJAA KUCHUKUA UBINGWA
Vardo
May 17, 2026
9:52 am
BAADA ya Yanga kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa kuiondoa JKT Tanzania, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kuwa hauhofia mpinzani yeyote watakayekutana naye hatua inayofuata, iwe ni Mashujaa FC au Azam FC.
Yanga leo itafahamu rasmi mpinzani wake wa nusu fainali baada ya mchezo wa robo fainali kati ya Mashujaa FC na Azam FC utakaopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, mshindi wa mchezo huo atakutana na mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania.
Akizungumza baada ya timu hiyo kufuzu hatua hiyo muhimu, msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kikosi hicho kipo tayari kwa changamoto yoyote inayokuja mbele yao huku akisisitiza kuwa morali ya wachezaji ipo juu kutokana na mwendelezo mzuri wa matokeo katika michezo ya hivi karibuni.
Kamwe amesema malengo ya Yanga msimu huu ni kuhakikisha wanatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, jambo ambalo limeifanya timu hiyo kuingia katika kila mchezo kwa umakini mkubwa bila kuchagua mpinzani.
“Ajaye yoyote awe Mashujaa FC au Azam FC tunamsubiri nusu fainali. Malengo yetu ni kutwaa ubingwa,” amesema Kamwe kwa kujiamini baada ya Yanga kufanikiwa kutinga hatua hiyo.
Kauli hiyo imeonyesha namna ambavyo benchi la ufundi, viongozi pamoja na wachezaji wa Yanga walivyojipanga kuhakikisha wanaendelea kupambana hadi mwisho wa mashindano hayo.
Mashabiki wa timu hiyo nao wameendelea kuonyesha matumaini makubwa wakiamini kikosi chao kina uwezo mkubwa wa kutwaa taji kutokana na ubora wa wachezaji pamoja na kiwango kizuri wanachoendelea kukionyesha msimu huu.