Habari za michezo

MNOGA ANA KIBARUA WEMBLEY

Vardo May 18, 2026 9:03 am

WAKATI winga wa Tanzania, Tarryn Allarakhia akifurahia kuipandisha daraja Rochdale AFC kutoka Ligi Daraja la Nne England maarufu National League kwenda League Two, bado Mbongo mwenzake, Haji Mnoga ana kibarua kizito nchini humo.

Mnoga anayekipiga Salford City inayoshiriki Ligi Daraja Tatu England maarufu League Two, sasa ana kibarua cha mechi ya fainali itakayotoa tiketi ya msimu ujao kucheza Ligi Daraja la Pili maarufu EFL League One.

Salford ilijikatia tiketi ya kucheza fainali ya playoff baada ya kuiondosha Grimsby Town katika michezo miwili yenye ushindani mkubwa ambapo ilishinda mabao 2-1 ugenini kabla ya kutoka sare ya 2-2 nyumbani.

Licha ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa League Two, Salford ilishindwa kupanda moja kwa moja kutokana na mfumo wa ligi hiyo unaozipa nafasi timu tatu za juu kupanda moja kwa moja huku timu zinazomaliza nafasi ya nne hadi saba zikicheza playoff kusaka nafasi ya kupanda daraja.

Mei 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Wembley jijini London, Salford City itakutana na Notts County katika mchezo wa fainali ya playoff utakaoamua nani atapanda daraja kwenda League One.

Salford City, moja ya klabu zinazomilikiwa na nyota wa zamani wa Manchester United, David Beckham, imejizatiti kuhakikisha inapanda daraja kucheza League One msimu ujao.

Beki huyo wa Tanzania amekuwa sehemu ya kikosi cha Salford ukiwa msimu wake wa pili uliokuwa na ushindani mkali, lakini ameendelea kuaminiwa kwenye kikosi cha kwanza.

Mnoga amekuwa mmoja wa wachezaji wa kuaminika Salford City, msimu huu akicheza mechi 26 kwa dakika 1,787, akianza mara 21.

Mchezaji huyo mwenye uwezo wa kucheza beki wa kulia, beki wa kati na winga wa kulia, ameonesha ubora mkubwa kwenye eneo la ulinzi, jambo lililomfanya kuwa sehemu muhimu katika mfumo wa kocha.

Akizungumzia nafasi yao, Mnoga amesema: “Ni kweli tulikosa kupanda moja kwa moja kwa tofauti ndogo, lakini sasa tuna lengo lingine la kutimiza, na ninaiona timu yetu ikifanikiwa. Nina imani kubwa sana na timu pamoja na kikosi tulichonacho.”

KILA MZUNGUKO UNAWEZA KUKUTOA NA KUKUPELEKA MBALI MRWANDA AFANYIWA MAJARIBIO YANGA PRINCESS