Habari za michezo
MRWANDA AFANYIWA MAJARIBIO YANGA PRINCESS
Vardo
May 18, 2026
9:14 am
YANGA Princess imeanza mchakato wa kuboresha kikosi hicho mapema kwa ajili ya msimu ujao na inaelezwa inamfanyia majaribio mshambuliaji wa Kamonyi WFC ya Rwanda, Sandrine Mutuyimana.
Hadi anaondoka kwao Rwanda mshambuliaji huyo alikuwa anaongoza kwa upachikaji mabao akiweka kambani 10 kwenye mechi nane.
Sandrine ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga na ndiyo sababu Yanga imeamua kumpa majaribio ili kuona kama anaweza kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Endapo benchi la ufundi la Yanga litaridhia, atasaini mkataba na kuwa mchezaji wa tatu kutoka Rwanda kucheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania,baada ya Jeaninne Mukandayisenga wa Yanga na Zawadi Usanase wa Simba Queens.
Katika kikosi cha Yanga mshambuliaji pekee wa kigeni anayebeba matumaini makubwa ya kufunga mabao ni Mukandayisenga, ambaye amekuwa tegemeo la timu hiyo katika mechi mbalimbali akiongoza kwenye orodha ya wafungaji akiweka kambani mabao 19 kwenye mechi 16 alizocheza.
Ujio wa Mutuyimana unatajwa kuwa mkakati wa kuongeza ushindani na kutoa msaada kwa Mukandayisenga, hasa kipindi ambacho Yanga Princess inajiandaa kuboresha kikosi.
Vyanzo vya karibu na klabu hiyo vimeeleza benchi la ufundi limevutiwa na uwezo wa Mutuyimana kutokana na uzoefu wake katika timu ya taifa ya Rwanda na uwezo wake wa kucheza kama mshambuliaji wa kati.
“Yupo karibu ana miezi miwili Tanzania na kwa taarifa nilizonazo, kocha ameridhika na uwezo wake na huenda mtamuona msimu ujao. Hata Mukandayisenga alisajiliwa baada ya kufanya majaribio kwa hiyo limekuwa mwendelezo,” kilisema chanzo hiko.
Mwanaspoti ilipomtafuta Mratibu wa Yanga, Kibwana Matokeo kufafanua kuhusu jambo hilo, lakini simu yake haikupatikana.