Habari za michezo

MESSI, RONALDO KATIKA FAINALI ZA MWISHO KOMBE LA DUNIA

Vardo May 21, 2026 9:07 am

NEW YORK, MAREKANI: KWA zaidi ya miaka 20 dunia ya soka imegawanyika katika makundi mawili makubwa, moja limeamini Lionel Messi ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea huku kundi jingine likisimama upande wa Cristiano Ronaldo kama mfalme wa kizazi hiki.

Mijadala, mabishano, takwimu, mataji na rekodi zimekuwa zikiwekwa na kuvunjwa na majina hayo mawili kwa zaidi ya miongo miwili huku dunia ikishuhudia ushindani mkubwa ambao haujawahi kutokea katika historia ya soka la kizazi hiki.

Sasa, dunia inaelekea kushuhudia mwisho enzi. Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinaweza kuwa za mwisho ‘Last Dance’ kwa Messi na Ronaldo kucheza mashindano hayo makubwa zaidi duniani, jambo ambalo tayari limeanza kuibua hisia tofauti kwa mashabiki wao.

Kwa miaka mingi, mastaa hao wawili wamevunja karibu kila rekodi inayowezekana, wamekusanya mataji ya kutosha tu, wamewahi kubeba timu zao katika nyakati ngumu na wamebadilisha kabisa namna dunia inavyouangalia mchezo wa soka.

MESSI NA SAFARI YAKE

Safari ya Messi katika Kombe la Dunia imekuwa kama filamu yenye maumivu, presha, lawama na mwisho furaha. Alianza kushiriki mashindano hayo 2006 nchini Ujerumani akiwa kijana mdogo mwenye ndoto kubwa za kuifuata njia ya Diego Maradona.

Katika mechi yake dhidi ya Serbia na Montenegro, Messi aliingia akitokea benchi na kufunga bao pamoja na kutoa asisti ndani ya dakika chache, jambo lililowafanya wengi waanze kuamini kuwa Argentina ilikuwa imepata mrithi halisi wa Maradona.

Hata hivyo, safari hiyo ya kwanza haikuisha kwa furaha kwani Argentina ilitolewa na Ujerumani katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 huku Messi akibaki benchi katika mchezo huo.

Miaka minne baadaye nchini Afrika Kusini mwaka 2010, matumaini yalikuwa makubwa zaidi kwa Messi kutokana na kiwango chake kikubwa akiwa FC Barcelona. Wengi waliamini huo ulikuwa wakati wake wa kung’ara katika Kombe la Dunia, lakini Argentina ilikumbana tena na jinamizi la Ujerumani baada ya kufungwa mabao 4-0 katika robo fainali.

Messi hakufunga bao lolote katika mashindano hayo licha ya kucheza vizuri. Lawama zilianza kumiminika kwake huku baadhi ya watu wakisema hawezi kuibeba Argentina kama alivyofanya Maradona mwaka 1986. Lakini pamoja na maneno hayo yote, Messi aliendelea kupambana huku akiamini siku moja angefika kileleni mwa dunia.

MAUMIVU KWA MESSI

Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil lilikuwa moja ya safari kubwa zaidi za Messi akiwa na Argentina. Katika mashindano hayo, alionyesha kiwango kikubwa sana kuanzia hatua ya makundi mpaka fainali.

Alifunga mabao katika kila mechi ya hatua ya makundi na kuibeba Argentina iliyokuwa na presha kubwa kutoka kwa mashabiki wake. Dunia ilianza kuamini kuwa huo ndio ulikuwa wakati wa Messi kuingia rasmi katika historia kama mchezaji mkubwa zaidi wa Argentina baada ya Maradona. Katika kila mchezo, alionekana kuwa mtu wa tofauti ndani ya kikosi hicho cha Argentina.

Lakini katika fainali dhidi ya Ujerumani, ndoto hiyo ilivunjika kwa maumivu makubwa. Argentina ilipoteza nafasi kadhaa muhimu huku Messi mwenyewe akikosa nafasi ya wazi ambayo wengi waliamini angeifunga kwa urahisi katika siku zake bora. Mwishoni mwa mchezo, Ujerumani ilishinda bao 1-0 kupitia Mario Gotze katika muda wa nyongeza.

Picha ya Messi akiwa anapita pembeni ya Kombe la Dunia huku akiwa mwenye huzuni ilibaki moja ya picha maarufu zaidi katika historia ya soka. Ingawa alishinda tuzo ya ‘Golden Ball’ kama mchezaji bora wa mashindano, machozi yake yalionyesha wazi kuwa tuzo hiyo haikuwa na maana mbele ya ndoto ya kunyanyua Kombe la Dunia iliyomponyoka tena.

MESSI ATIMIZA NDOTO

Baada ya miaka mingi ya maumivu, lawama na kushindwa kufika kileleni, Messi aliingia katika Kombe la Dunia la 2022 akiwa na presha kubwa, wengi waliamini hiyo ilikuwa nafasi yake ya mwisho kushinda taji hilo kubwa zaidi duniani.

Argentina ilianza vibaya mashindano hayo baada ya kufungwa na Saudi Arabia, jambo lililozua taharuki kubwa duniani. Lakini kuanzia hapo, Messi aligeuka kuwa kiongozi halisi wa timu hiyo.

Alifunga mabao muhimu dhidi ya Mexico, Australia, Uholanzi, Croatia na Ufaransa huku akiwa katika kiwango bora.

Katika fainali dhidi ya Ufaransa, Messi alitoa moja ya maonyesho makubwa zaidi kuwahi kuonekana katika historia ya Kombe la Dunia.

 Alifunga mabao mawili ndani ya mchezo huku akiongoza Argentina katika mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.Baada ya ushindi wa penalti 4-2, dunia ilishuhudia picha ambayo mashabiki wa soka walikuwa wameisubiri kwa miaka mingi, Messi akiinua Kombe la Dunia.

Ushindi huo ulimfanya kukamilisha kila kitu katika soka. Alishinda Copa America, Finalissima na hatimaye Kombe la Dunia. Kwa wengi, huo ulikuwa wakati rasmi ambao ulimfanya kuingia juu kabisa katika mjadala wa mchezaji bora kuwahi kutokea duniani.

SAFARI YA RONALDO

Kwa upande wa Cristiano Ronaldo, safari yake katika Kombe la Dunia imekuwa tofauti kabisa, lakini yenye presha kubwa sawa na ya Messi. Ronaldo alianza kushiriki mashindano hayo mwaka 2006 akiwa kijana mwenye kasi kubwa na uwezo wa ajabu wa kufunga mabao.

Katika mashindano hayo nchini Ujerumani, aliisaidia Ureno kufika nusu fainali, hatua ambayo bado ni moja ya mafanikio makubwa zaidi ya taifa hilo katika historia ya Kombe la Dunia. Ronaldo alionyesha kiwango kizuri na kuanza kujijenga kama mmoja wa wachezaji bora duniani.

Hata hivyo, miaka iliyofuata haikuwa rahisi kwake katika mashindano hayo makubwa. Ureno mara nyingi ilionekana kutokuwa na kikosi chenye nguvu sawa na mataifa makubwa kama Argentina, Brazil, Ufaransa au Ujerumani. Ronaldo alibeba mzigo mkubwa wa matumaini ya taifa lake kwa muda mrefu sana.

Katika Kombe la Dunia 2010, 2014 na 2018, Ureno ilishindwa kufika mbali licha ya uwepo wake. Mara nyingi alikabiliwa na lawama kutoka kwa mashabiki waliotaka kumuona akiibeba nchi yake hadi ubingwa wa dunia kama alivyofanya katika ngazi ya klabu.

MAUMIVU YA QATAR

Wakati Messi akiandika historia nchini Qatar, upande wa Ronaldo mambo yalikuwa tofauti kabisa. Mashindano hayo yaligeuka kuwa moja ya vipindi vigumu zaidi katika maisha yake ya soka.

Kabla ya Kombe la Dunia kuanza, tayari alikuwa kwenye mgogoro mkubwa na Manchester United FC baada ya mahojiano yake yaliyotikisa. Alifika Qatar akiwa na presha kubwa huku wengi wakihisi kuwa huo ungekuwa mwisho wa zama zake.

Katika mashindano hayo, Ronaldo alianza vizuri kwa kufunga dhidi ya Ghana na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika Kombe la Dunia la tano tofauti. Hata hivyo, kadri mashindano yalivyoendelea alipoteza nafasi yake ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Ureno. Kocha Fernando Santos alianza kumweka benchi katika baadhi ya michezo muhimu, jambo lililozua mjadala mkubwa duniani.

Ureno ilitolewa na Morocco katika robo fainali na Ronaldo alionekana akilia machozi wakati akitoka uwanjani. Picha hiyo ilisimama kama ishara ya maumivu makubwa ya mchezaji ambaye alikuwa ametumia maisha yake yote kujaribu kuifikisha Ureno kileleni lakini hakufanikiwa.

REKODI KUBWA ZILIZOWEKWA

Katika historia ya soka duniani, hakuna ushindani uliowahi kuzalisha rekodi nyingi kama ule wa Messi na Ronaldo.  Messi ana rekodi ya Ballon d’Or nane huku Cristiano Ronaldo akiwa na tano. Wote wawili wamefunga zaidi ya mabao 800 katika maisha yao ya soka, jambo ambalo halijawahi kufanywa na wachezaji wengi katika historia ya mchezo huo.

Katika Kombe la Dunia, Messi ameweka rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi akiwa na mechi 26 pamoja na kuwa mchezaji mwenye tuzo nyingi zaidi za mchezaji bora wa mechi ‘Man of the Match’.

Pia ndiye mchezaji pekee aliyefunga katika kila hatua ya mashindano ndani ya Kombe la Dunia moja.

Ronaldo ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga katika fainali  tano tofauti.

Wote wawili pia wamecheza Kombe la Dunia kwa mara sita, jambo ambalo linaonyesha uimara wao wa kipekee kwa zaidi ya miaka 20. Rekodi hizo zinaifanya dunia kuamini kuwa ushindani wao huenda usitokee tena.

LAST DANCE 2026

Japo waswali wanapenda kusema kuwa umri ni namba ila sio rahisi kwa Messi mwenye miaka 39 na Ronaldo mwenye 41 kuwa sehemu ya vikosi vyao katika fainali zijazo za Kombe la Dunia, hali inayofanya wengi kuamini kuwa huo utakuwa mwisho wao katika mashindano hayo makubwa.

Ingawa bado wanaendelea kucheza katika kiwango kizuri, muda unaonekana kuwa upande ambao hakuna mwanadamu anaweza kuushinda.  Ndiyo maana mashindano hayo yanaitwa “Last Dance” ya mastaa hao.

Hisia za mashabiki zimekuwa kubwa kutokana na ukweli kwamba baada ya wao kuondoka, dunia ya soka itaingia katika zama mpya kabisa.

Vijana kama Kylian Mbappe na Lamine Yamal wanaonekana kuwa sura mpya za kizazi kijacho, lakini wengi bado wanaamini kuwa haitakuwa rahisi kuona ushindani mwingine mkubwa kama ule wa Messi na Ronaldo.

UKWELI MTUPU

Bila kujali nani anaonekana bora zaidi kati yao, jambo moja ambalo halina ubishi ni kwamba Messi na Ronaldo wamebadilisha kabisa historia ya mchezo wa soka. Wameweka viwango vipya vya ushindani, nidhamu, kujituma na mafanikio.

Wameonyesha kuwa vipaji vikubwa vinaweza kudumu kwa muda mrefu ikiwa mtu atakuwa tayari kujituma kila siku. Kutoka katika viwanja vya Hispania mpaka Uingereza, Italia, Ufaransa, Marekani na Saudi Arabia, majina yao yameendelea kutikisa dunia.

Je, Messi ataweza kuiongoza Argentina kutetea ubingwa wake wa dunia au Ronaldo ataandika hadithi ya mwisho ya kishujaa akiwa na Ureno?

NABI AENDELEA KUTAKA FEI TOTO KUCHEZA KIMATAIFA MVUTANO WA MBAPPE, VINI BALAA REAL MADRID