Habari za michezo

MVUTANO WA MBAPPE, VINI BALAA REAL MADRID

Vardo May 21, 2026 9:12 am

MADRID, HISPANIA: MVUTANO unaoizunguka Real Madrid sasa hauhusiani tena tu na matokeo mabaya uwanjani, lakini kuna mgawanyiko unaoendelea miongoni mwa nyota wawili wa kikosi hicho, Kylian Mbappe na Vinicius Junior ambao kwa sasa umegeuka kuwa gumzo kubwa.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Hispania, mgawanyiko huo unaanza kufanana na vita vya kugombea madaraka kati ya wachezaji hao unaoweza kusababisha matatizo makubwa ya muda mrefu ndani ya klabu hiyo kubwa zaidi ya soka duniani.

Kwa miezi kadhaa, maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu kwanini mastaa hao wawili wenye uwezo mkubwa wa kushambulia wameshindwa kuendana kikamilifu uwanjani na sasa inaeleza kuwa kuna matatizo makubwa zaidi kuliko mbinu au kutoelewana.

Mtangazaji maarufu wa televisheni nchini Hispania, Josep Pedrerol, amekaririwa kupitia kipindi cha El Chiringuito de Jugones kwamba upande wa Mbappe unaamini Vinicius Jr amekuwa akivumisha taarifa mbaya kwa vyombo vya habari ili kuonyesha Mbappe ndiye chanzo cha hali mbaya inayokabaliana nayo klabu hiyo katika ligi kwa sasa.

Pedrerol alisema Mbappe anahisi Vinicius alikuwa na mchango mkubwa katika kumshawishi aliyekuwa kocha wao, Xabi Alonso kuondoka klabuni mwezi Januari na hivyo siyo mtu sahihi kuendelea kubaki katika kikosi hicho.

Kama madai hayo ni ya kweli yatakuwa yanaonyesha kiwango kikubwa cha mgogoro ndani ya chumba cha kubadilishia nguo cha timu hiyo, ambapo umekuwa msimu mgumu kwa klabu hiyo kuanzia mazoezini, ongezeko la hasira kutoka kwa mashabiki na hata mkutano wa dharura na waandishi wa habari uliofanywa na rais wa klabu Florentino Perez, ambaye alijibu hadharani ukosoaji na kuitisha uchaguzi wa urais huku akitetea uongozi wake.

Malalamiko dhidi ya Mbappe hayahusiani na kiwango chake cha uchezaji, lakini ushawishi na Vinicius anadaiwa kudai kwamba ujio wa mchezaji huyo haukuzingatia uhalisia, kwani kikosi hicho tayari kilikuwa na mastaa wengi wakubwa wa maana ambao wangeendelea kukipa mafanikio ndani na nje ya uwanja

Kabla ya Mbappe kujiunga na kikosi hicho kilionekana kuwa na mfumo mzuri zaidi wa ushambuliaji uliokuwa ukiongozwa na Vinícius Jr, Jude Bellingham na Rodrygo ambao waliisaidia kutwaa taji lake la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku kikionyesha mshikamano mkubwa na uwiano mzuri wa kiulinzi.

Licha ya Mbappe na Vinícius kufunga zaidi ya mabao 60 kwa pamoja msimu huu, ushirikiano wao pia unaonekana kuwa na matatizo nyakati fulani, ambapo wote wawili hupendelea kucheza upande wa kushoto, jambo linalowafanya mara nyingi kuingia maeneo yaleyale na kuvuruga mpangilio wa timu. Katika mashindano yote msimu huu wamefunga katika mchezo mmoja mara sita pekee.

MESSI, RONALDO KATIKA FAINALI ZA MWISHO KOMBE LA DUNIA DAKIKA 50 ZAMTOSHA NEYMAR KUVUTA MABILIONI