KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema bado hajakata tamaa kufanya kazi na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum akiamini muda wake kwenda kuongeza thamani nje ya Tanzania umefika.
Ikumbukwe kwamba, Nabi aliwahi kufanya kazi na Fei Toto msimu mmoja na nusu kabla ya kiungo huyo kusitisha mkataba Yanga na kutua Azam alipo ukiwa ni msimu wa tatu.
Baada ya kuondoka kwa Fei Toto ndani ya Yanga 2022-2023, Nabi naye alimaliza safari yake klabuni hapo alipofanya kazi kuanzia Aprili 2021 hadi Juni 2023, akiifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara.
Mtunisia huyo alipomalizana na Yanga, alitua AS FAR ya Morocco aliyoinoa msimu mmoja kabla ya kwenda Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo aliifundisha 2024/25, lakini katika timu zote hizo hakuwahi kuacha kutaka huduma ya Fei.
Akizungumza na Soka la Bongo, Nabi alisema kama akipata timu nyingine ataendelea kumuhitaji Fei kwa kuwa anaamini sana uwezo wake na anatamani kumuona akicheza nje ya Tanzania.
“Moja ya viungo bora Tanzania ni Fei, kumuacha aendelee kucheza ligi ya ndani ni kama kumfanya mdogo, kwa sababu sasa hivi anatakiwa kujulikana kimataifa, si hivyo tu, mchezaji mkubwa lazima apate changamoto mpya.
“Kwa sasa Fei anaijua vizuri ligi ya ndani, hakuna kocha anaweza kupanga kikosi asimweke, lakini ni muda wa dunia kujua Tanzania ina mchezaji mwenye kiwango kikubwa kama Fei,” alisema Nabi.
“Bado sijakata tamaa, natamani siku moja kufanya naye kazi au kumuona Fei Toto akicheza soka nje ya Tanzania ili kuongeza thamani yake kimataifa. Kauli yangu haina maana kwamba Fei Toto hastahili kuichezea Azam FC, lakini shauku yangu ni kumuona anatamba kimataifa.”
Fei ameichezea Azam FC kwa misimu mitatu na bado ana mkataba na klabu hiyo hadi 2027.
Msimu wa kwanza 2023-2024 akiwa Azam, Fei alifanya vizuri akimaliza ligi na mabao 19, nyuma ya kinara Aziz KI aliyekuwa na 21, kisha 2024-2025 akafunga manne, lakini akaibuka kinara wa asisti Ligi Kuu akiwa nazo 13, huku msimu huu 2025-2026 akiongoza na mabao 11, pia ana asisti nane.