AZAM FC imeendelea kusuka kikosi chake kuelekea msimu ujao, ambapo sasa iko hatua za mwisho kumnasa winga wa FC Saint-Éloi Lupopo, Henoc Molia, baada ya mapendekezo ya kocha Florent Ibenge.
Azam ilituma ujumbe maalum DR Congo kwa ajili ya kumfuatilia mchezaji huyo na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na upande wake ili kuangalia namna ya kumpata.
Ibenge katika ripoti yake alimtaja Molia kama mchezaji sahihi kwa mfumo anaoutaka, akiamini anaweza kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, Ibenge alimtaka Molia kwa sababu ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kuamua mechi, ana kasi na anafit kabisa kwenye falsafa ya kocha.
“Molia amekuwa kwenye kiwango bora akiwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Lupopo kutokana na uwezo wake wa kucheza pembeni kwa kasi, kutengeneza nafasi na kufunga mabao jambo lililovutia vigogo mbalimbali kuhitaji saini yake.
“Ibenge ndiye anaemtaka mchezaji huyo kwa ajili ya kuimarisha kikosi hicho kwa ajili kuelekea msimu mpya
Azam imekuwa kwenye mpango wa kukiboresha kikosi chake mapema ili kuingia na nguvu kubwa kwenye mashindano ya ndani na yale ya kimataifa msimu ujao.
Mazungumzo kati ya Azam na upande wa mchezaji huyo yameelezwa kuingia hatua nzuri na kuna matumaini makubwa ya kufanikisha dili hilo ndani ya muda mfupi ujao.
Azam FC inaendelea kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao ikiwa na lengo la kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani na kimataifa chini ya uongozi wa Ibenge.