Habari za michezo
SIMBA WASEMA MAFANIKIO YA CHAMA NI HESHIMA KWA TANZANIA SIO KLABU PEKEE
Vardo
May 21, 2026
8:52 am
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameibua mjadala mpya baada ya kueleza kuwa kuna dalili za Yanga SC kuonyesha wivu kufuatia sifa kubwa zinazotolewa kwa bao la kiungo wa Simba, Clatous Chama, ambalo limeendelea kuzungumzwa ndani na nje ya Tanzania.
Chama alifunga bao hilo la kuvutia katika mchezo wa Kariakoo Derby uliopigwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Isamuhyo dhidi ya Yanga SC, bao ambalo limeendelea kupata umaarufu mkubwa kwenye mitandao na majadiliano ya soka kimataifa.
Miongoni mwa watu waliolizungumza zaidi bao hilo ni gwiji wa soka duniani Rio Ferdinand, ambaye alitembelea Tanzania hivi karibuni katika ziara ya mazungumzo ya maendeleo ya michezo na uwekezaji.
Akiwa nchini, Ferdinand alionyeshwa video ya bao hilo na kulisifia kuwa ni la kiwango cha juu sana, akisema linaweza hata kuwania tuzo ya kimataifa kama Puskás kutokana na ubora wake wa kiufundi na uamuzi wa haraka wa mfungaji.
Kauli hiyo imezua mijadala mikubwa mitandaoni, ambapo mashabiki wa soka wamegawanyika, baadhi wakilishangilia bao hilo huku wengine wakitafsiri sifa hizo kama sehemu ya ushindani mkali wa mitaani kati ya Simba na Yanga.
Ahmed amesema hakuna ubaya kwa mgeni wa kimataifa kusifia kipaji kinachoonekana uwanjani, akisisitiza kuwa mafanikio ya Chama yanapaswa kuonekana kama heshima kwa soka la Tanzania kwa ujumla.
“Popote linapozungumzwa goli la Chama kuna mambo matatu yanatajwa: ligi ya Tanzania, Tanzania yenyewe na Simba SC. Hii ni heshima kwa nchi, si kwa klabu moja tu,” amesema Ahmed.
Aliongeza kuwa baadhi ya watu wamechukulia vibaya sifa hizo kutokana na hisia za ushindani wa ndani, akisisitiza kuwa mafanikio ya wachezaji wa Ligi Kuu yanapaswa kuleta furaha badala ya malumbano yasiyoisha.
Simba SC kwa upande wao wamesema wanaridhishwa na pongezi hizo, wakieleza kuwa zinathibitisha ubora wa Clatous Chama na mchango wake mkubwa katika kuipa ligi ya Tanzania heshima ya kimataifa.