Habari za michezo

MZAMIRU AFUNGUKA MAISHA MAPYA TRA UNITED BAADA YA SIMBA

Vardo May 21, 2026 8:41 am

KIUNGO wa kati, Mzamiru Yassin ameendelea kuvuta hisia za mashabiki baada ya kufunguka kuhusu maisha yake mapya ndani ya kikosi cha TRA United, akieleza namna anavyoendelea kuzoea mazingira mapya baada ya kuondoka kwenye presha ya klabu kubwa.

Mzamiru, ambaye aliwahi kuwa miongoni mwa viungo tegemeo ndani ya Simba SC, amesema tofauti ya mazingira imekuwepo, lakini amesisitiza kuwa TRA United imekuwa sehemu yenye utulivu na inayompa nafasi ya kucheza soka kwa uhuru zaidi.

Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo msimu huu, kiungo huyo amesema malengo yao makuu ni kuhakikisha wanapambana kwa kila hali ili kusogea juu kwenye msimamo wa ligi, huku wakilenga kumaliza ndani ya nafasi nne bora.

“Tunaendelea kusukuma ili tupambane tumalize nafasi za juu ikiwemo nafasi ya nne,” amesema Mzamiru, akionesha dhamira ya kikosi hicho kutaka kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Ameongeza kuwa ushindani uliopo ndani ya ligi unawahitaji kuwa makini kila mchezo, akibainisha kuwa hakuna mechi rahisi na kila pointi ina umuhimu mkubwa kwa malengo yao.

Kwa upande wa maisha yake binafsi ndani ya klabu, Mzamiru ameeleza kuwa bado ana mkataba na TRA United na kwa sasa hana mpango wa kuondoka, akisisitiza kuwa ameridhishwa na mazingira mapya aliyoyakuta.

“Bado nipo TRA United ni maisha mazuri licha ya kuwa tofauti na Simba, ila kwa sasa ninafuraha na hapa na nina imani nitaendelea kuwepo,” ameongeza kiungo huyo.

Kauli yake imepokelewa kwa matumaini makubwa na mashabiki wa TRA United, ambao wanaamini uwepo wake utaongeza uimara katika eneo la kiungo na kusaidia timu kupigania malengo yao ya msimu huu.

FEI TOTO AWA ZAWADI ADIMU LIGI KUU VITA YA USAJILI YAPAMBA MOTO SIMBA WASEMA MAFANIKIO YA CHAMA NI HESHIMA KWA TANZANIA SIO KLABU PEKEE