Habari za michezo

MAGEUZI YA BARKER YAIFANYA SIMBA SC KUONEKANA TENA YA KUTISHA

Vardo May 22, 2026 10:37 am

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameendelea kuvuna sifa kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka nchini kutokana na namna alivyoibadilisha timu hiyo kwa muda mfupi tangu alipowasili Msimbazi.

Barker amekuwa akifanya kazi kwa utulivu mkubwa, bila kelele nyingi wala presha za nje ya uwanja, huku akionyesha uwezo mkubwa wa kuirejesha Simba kwenye ushindani na hadhi yake ya kawaida ndani ya soka la Tanzania.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini ameonekana kuja na falsafa ya utulivu, umakini na matokeo, jambo ambalo limeanza kuonekana wazi ndani ya kikosi hicho kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tangu achukue mikoba ya kuinoa Simba, Barker ameweza kujenga timu yenye ushindani mkubwa, morali ya juu na nidhamu ya mchezo, huku wachezaji wakionekana kucheza kwa kujiamini na kupambana kwa nguvu katika kila mechi.

Miongoni mwa mafanikio yake makubwa hadi sasa ni kuiongoza Simba kutwaa Kombe la Muungano baada ya kuifunga Yanga kwenye mchezo wa fainali uliokuwa na ushindani mkubwa na hisia kali kutoka kwa mashabiki wa timu hizo kongwe nchini.

Mbali na hilo, Barker alikaribia kuondoka na ushindi kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Young Africans SC kabla ya bao la Mwalimu kufutwa kwa madai ya kuotea.

Tukio hilo liliwaacha wengi wakiamini kuwa Simba ilikuwa imeanza kupata sura mpya chini ya benchi hilo la ufundi.
Katika mchezo wa marudiano wa Kariakoo Derby, Simba iliibuka na sare dhidi ya wapinzani wao wa jadi, mechi iliyokuja katika kipindi kigumu kwa Yanga na baadaye kuchangia mabadiliko ndani ya benchi lao la ufundi baada ya klabu hiyo kuachana na kocha wake.

Kwa sasa, Simba imefanikiwa kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo linaloonyesha wazi kuwa timu hiyo ipo kwenye njia nzuri ya kurejesha heshima yake na kupigania ubingwa hadi dakika ya mwisho wa msimu.

Kauli inayozidi kupewa nguvu na mashabiki wengi ni kwamba Barker hafanyi siasa wala drama nyingi, bali anaamini kwenye kazi, mipango na matokeo.

Utulivu wake pembeni mwa uwanja umeonekana kuwa moja ya silaha kubwa iliyoirudisha Simba kwenye ushindani mkubwa wa taji.

Sasa macho na masikio ya mashabiki wengi wa soka nchini yameelekezwa kwa Barker kuona kama ataweza kuimalizia kazi aliyoianza kwa kuiongoza Simba kutwaa ubingwa wa ligi na kuandika historia mpya ndani ya klabu hiyo yenye mashabiki wengi nchini

VASO PSYCHO INAPELEKA BURUDANI HATUA NYINGINE CHAMA AIGEUZA MEI KUWA MALI YAKE SIMBA