MECHI ya Ligi Kuu Bara kati ya Namungo dhidi ya Mbeya City, imeshindwa kutoa mshindi, baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikifungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Wenyeji Namungo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza, mfungaji akiwa kiungo Salum Kabunda kwa shuti kali dakika ya sita akiunasa mpira uliookolewa kwa kichwa na beki wa City, Kelvin Pemba.
Dakika ya 28, Mbeya City ikafanikiwa kusawazisha kwa bao zuri mfungaji akiwa mshambuliaji wa timu hiyo na nahodha, Eliud Ambokile akiunasa mpira wa krosi ndefu kutoka kwa beki wa kushoto, Yahya Mbegu.
Namungo itajilaumu yenyewe kukosa ushindi kwenye mchezo huo na lawama zitamuangukia mshambuliaji wao Heritier Makambo ambaye dakika ya 42 akipoteza nafasi ya wazi kumalizia kwa kufunga, akishindwa kumalizia mpira alipounasa akiwa mbele ya kipa Sudi Dondola.
Dakika ya 90+1, Dondola akafanya kazi nyingine bora akiokoa mpira wa kichwa cha mshambuliaji Fabrice Ngoy kilichokuwa kinaelekea ndani na kuwa kona, shambulizi lililowapelekea benchi zima la Namungo kushangaa wakiamini timu yao inapata bao la pili.
Dondola tena ambaye ametangazwa kuwa nyota wa mchezo huo akafanya kazi nyingine bora akiokoa shuti kali la kiungo Jacob Masawe dakika ya 90+4 Namungo ikipoteza nafasi nyingine nzuri ya kupata bao la ushindi.
Kipindi cha kwanza Mbeya City ilionekaba kucheza vizuri ikitawala mchezo huo lakini Namungo nayo ikafanya hivyo kipindi cha pili huku safu za ushambuliaji kwa timu zote zikionyesha kukosa makali ya kumalizia mashambulizi.
Matokeo hayo yanaifanya Namungo kuendelea kusalia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 25 huku Mbeya City nayo ikiwa chini yake kwenye nafasi ya 14 na pointi 22, zote zikicheza mechi 24.