“Haitakuwa mechi rahisi, lakini tupo tayari kwa ushindani kuhakikisha tunavuna pointi tatu, pia tunahitaji nguvu ya mashabiki kuja kutusapoti kwa wingi ili kutupa motisha zaidi.”
Kwa Singida Black Stars iliyopo nafasi ya nne katika msimamo kabla ya mechi za jana, imecheza mechi 23, imeshinda 11, sare tano, imepoteza saba, ikivuna pointi 38, endapo ikishinda dhidi ya Yanga leo itafikisha pointi 41 na kuendelea kusalia nafasi hiyo.
Kocha wa Singida BS, Muhibu Kanu amesema kuwa mechi hiyo imebeba vita ya nafasi katika msimamo wa ligi, hivyo ushindi utakuwa umeiweka kwenye nafasi nzuri ya kurejea kwenye michuano ya kimataifa.
“Tangu nakabidhiwa timu nilisema tunahitaji kupata nafasi ya kucheza michuano ya CAF, hivyo tunahitaji ushindi ili kuendelea kulinda nafasi ya nne tuliyopo na ikibidi kuipambania ya tatu. Lakini pia mechi ya Mei 5 tulifungwa na Yanga kwa mabao 3-0, hivyo hatutataka kuendeleza kipigo hicho.”
Leo mabeki wa Singida wana kibarua cha kuwakabili washambuliaji hatari wa Yanga waliohusika na mabao mengi kama Prince Dube aliyefuga tisa na asisti tatu, bila ya kuwasahau viungo wanaofanya vizuri kama Pacome Zouzoua (mabao saba, asisti nne), Mudathir Yahya (mabao saba) na Allan Okello (mabao saba na asisti saba).
Jicho la Singida litakuwa hapo kwani mastaa hao ndiyo waliyokuwa wamewaadhibu mara ya mwisho walipokutana kwa kipigo cha mabao 3-0 ambapo Dube alifunga dakika ya 39, Okello kwa penati dakika ya 45 na Mudathir dakika ya 55.
Kwa upande wa safu ya ulinzi ya Yanga ikiongozwa na kipa Djigui Diarra mwenye cleansheets 13, itakuwa na kazi ya kuwalinda nyota wa Singida wasiwe na madhara hasa mshambuliaji Mossi Ndumumwe mwenye mabao manane. Mbali na huyo, kuna beki Ibrahim Imoro mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza pasi za mabao akiwa nazo nne na kufunga matatu, pia kiungo Emmanuel Keyekeh mwenye mabao matatu.
Wakati vita ya wawili hao ikimalizika, saa 12:30 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, Azam FC itaikaribisha Tanzania Prisons ambayo itakuwa na presha zaidi ya kuhitaji ushindi ili kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja, katika mechi 23 ilizocheza, Tanzania Prisons imeshinda nne, sare tano, imepoteza 14, ikivuna pointi 17, hivyo ikishinda itafikisha alama 20 ambazo hazitaiondoa kwenye nafasi ya 15 iliyopo sasa.
Kwa Azam, tamanio lao kubwa ni kushinda ili kusogelea nafasi mbili za juu kwani hivi sasa ni ya tatu na pointi 46 ilizozipata katika mechi 23, ikishinda 12, sare 10, imepoteza moja.
Kocha wa Azam, Florent Ibenge, amesema ni muhimu kushinda na jambo analolitaka kwa wachezaji ni kuwa na morali ya juu kama wanayoitumia wakicheza na Simba na Yanga.
“Mechi zote ni muhimu iwe tumecheza na Prisons, TRA, Singida BS kila timu tunahitaji kuvuna pointi tatu,” amesema.
Kwa upande wa kocha wa Prisons, Shadrack Nsajigwa, amesema: “Tumekuwa na siku tatu za kufanya mazoezi, unapokutana na timu kama Azam yenye mbinu nzuri na kiwango cha juu, lazima uwaandae wachezaji kiakili zaidi, ingawa kimbinu tupo vizuri, itakuwa mechi ngumu, maana mechi tuliyocheza Mbeya tuliyocheza Mei 5 tulisuluhu.”
Kwa mabeki wa Prisons nyota wa Azam wanaotakiwa kuwachunga zaidi ni kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliye na mabao 11 na asisti nane akiwa kinara wa takwimu hizo zote, mwingine ni Idd Seleman aliyefunga mabao saba na asisti tatu na Jephte Kitambala mwenye mabao sita, upande wa Prisons wachezaji ambao watatakiwa kuchungwa ni George Mpole aliyefunga mabao matano na Oscar Mwajanga mwenye mabao mawili.