Habari za michezo

CARRICK AIPONGEZA ARSENAL, AKITHIBITISHA KUPEWA MKATABA WA KUDUMU MAN UNITED

Vardo May 22, 2026 12:24 pm

Kocha wa mpito wa Manchester United, Michael Carrick, amethibitisha kwa vitendo kuwa atateuliwa kuwa kocha mkuu wa kudumu wa klabu hiyo, huku tangazo rasmi likicheleweshwa na mchakato wa kukamilisha mikataba ya benchi lake la ufundi.

Klabu hiyo inatarajia kutoa taarifa hiyo rasmi kabla ya mchezo wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Brighton keshokutwa Jumapili, ingawa kuna uwezekano ikasubiriwa hadi wiki ijayo.

Carrick mwenyewe amefunguka kuwa kuhusu mustakabali wake utakuwa wazi ndani ya siku chache zijazo, akieleza kuwa kila kitu kiko hatua za mwisho kabisa kukamilika.

Katika hatua nyingine, Carrick ametumia fursa hiyo kuwapongeza wapinzani wao Arsenal kwa kufanikiwa kukata kiu ya miaka 22 ya kukosa taji la Ligi Kuu ya England wiki hii.

Arsenal imekuwa klabu ya tano tofauti kutwaa ubingwa huo tangu Manchester United iliponyanyua ndoo hiyo kwa mara ya mwisho mnamo mwaka 2013. Carrick amemsifu kocha Mikel Arteta, wachezaji, na wafanyakazi wa Arsenal kwa uvumilivu na maendeleo makubwa waliyoonyesha kwa miaka kadhaa hadi kufikia hatua ya kustahili ubingwa huo.Kuhusu mustakabali wa Manchester United, Carrick amesisitiza kuwa klabu hiyo inapambana kurudi katika ubora haraka iwezekanavyo. Ingawa uongozi wa klabu hiyo umelenga kutwaa taji ifikapo mwaka 2028, kumaliza katika nafasi ya tatu msimu huu kumewapa mashabiki matumaini makubwa ya kupambania ubingwa msimu ujao. Kocha huyo amebainisha kuwa tayari wana msingi mzuri wa kikosi chenye mchanganyiko wa umri tofauti, na kuongeza kuwa safu yao ya ushambuliaji ni hatari na inaleta msisimko mkubwa kuelekea msimu ujao.

HARMONIZE, MARIOO KUACHA KUACHIA KOLABO NYINGINE YA MOTO MECHO ZA KIBINGWA YANGA, AZAM