Habari za michezo
HARMONIZE, MARIOO KUACHA KUACHIA KOLABO NYINGINE YA MOTO
Vardo
May 22, 2026
12:18 pm
Ingawa hawafanyi kazi kama kundi la muziki, lakini mfululizo wa ngoma kali kutoka kwa Harmonize na Marioo, unatoa picha ya jinsi wasanii hao walivyounganisha muziki wao.
Harmonize, mwanzilishi wa Konde Music Worldwide na Marioo kutokea Bad Nation Label, wametengeneza nyimbo nyingi ambazo zimewabamba vilivyo mashabiki wao.
Wiki hii wawili hao wamethibitisha ujio wa kolabo yao nyingine ambayo inatayarishwa na Kaniba Creator ambaye miaka ya hivi karibuni nyimbo nyingi zinazopita katika mikono yake zimekuwa zikifanya vizuri.
Tayari mastaa hao wameachia kolabo zao nne ambazo ni: Naogopa (2022), Away (2024), Disconnect (2024), Wangu (2024), huku moja, Pere (2025) wakishirikishwa wote na Rayvanny kutokea Next Level Music (NLM).
Meneja wa Harmonize na Konde Music kwa jumla, Sandra Brown ameitaja kolabo hiyo mpya kuwa ya viwango vya juu na ni mwendelezo wa kile ambacho tayari wasanii hao wamekifanya.
“Nilikutana na vijana studio, kwa kweli nilitaka tu kusalimia na kuondoka lakini nikaamua kubaki na niseme tu huu wimbo mpya ni wa moto sana,” ameeleza na kuongeza.
“Nazipenda sana kolabo za Marioo na Harmonize, kuna mchanganyiko (chemistry) halisi wa muziki kati yao. Nina shauku kubwa ya kutaka kuusikia ukiwa umetoka. Hongera Kaniba Creator,” aliandika Sandra Instagram.
Ushirikiano huo mpya umekuja siku chache baada ya Harmonize kutangaza ujio wa albamu yake ya sita ambayo kwa mujibu wa maelezo yake imelenga soko la kimataifa (global album) zaidi.
Utakumbuka mwishoni mwa mwaka uliopita Harmonize alipanga kuachia albamu yake aliyoipa jina la “31” lakini hakufanya hivyo, kwa hiyo tutegemee kitu kizuri zaidi baada ya maandalizi ya muda mrefu.
Kwa mujibu wa Harmonize, albamu hii ya sita ameiandaa kwa utulivu mkubwa kiasi kwamba anaamini ina hadhi ya kushinda tuzo kubwa za muziki duniani ikiwemo Grammy ambazo zilianza kutolewa miaka 67 iliyopita.
Harmonize anayetamba kwa sasa na wimbo wake, Wewe (2026), tayari ameachia albamu zake tano ambazo ni – Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024).
Tatu kati ya hizo zilichaguliwa kuwania Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) huku moja ikishinda ambayo ni Visit Bongo (2023).
Ushindi huo ulikuja baada ya kuzibwaga albamu nyingine kama – ‘5’ ya Abigail Chams, ‘Swahili Kid’ ya D Voice, ‘Most People Want This’ ya Navy Kenzo, na ‘Flowers III’ ya Rayvanny.
Ikumbukwe kabla ya Harmonize kuanza kutoa mfulizo wa albamu, alianza na EP, Afro Bongo (2019) iliyobamba sana kutokana na kushirikisha wasinii wazito kama Diamond Platnumz, Yemi Alade, Mr. Eazi na Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021.
Hivyo iwapo Marioo atasikika katika albamu mpya ya Harmonize, ni wazi kuwa ushirikiano huo atatoa matokeo chanya zaidi katika mradi huo kutokana na nguvu ya ushawishi ya Marioo katika soko la muziki kwa sasa.
Katika kipindi hiki ambacho kipimo cha wimbo au albamu kufanya vizuri ni kiwango cha namba ilichopata katika majukwaa ya kidijitali (digital streaming), tunaweza kusema Marioo ni miongoni mwa wasanii sahihi kabisa kuwepo katika albamu hiyo ya Harmonize.
Utakumbuka kolabo yao ya kwanza, Naogopa (2022), hadi sasa ndio wimbo wa Marioo ambao umefanya vizuri zaidi YouTube na video yake imeshatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 66.8 ikiwa ni takribani miaka minne tangu imeachiwa.
Katika albamu ya pili yake Marioo, The God Son (2024) ambayo ilifanya vizuri sana hasa mtandaoni, Harmonize naye alikuwa na mchango wake katika mradi huo kwa sababu alishirikishwa katika wimbo mmoja (Wangu) ambao video yake imeshatazamwa YouTube mara milioni 19.2.
Mbali na Marioo, wasanii wengine ambao Harmonize ameshirikiana nao mara nyingi na kazi hizo kuwa na matokeo makubwa ni pamoja na Ibraah, Anjella na Abigail Chams.
Mathalani baada ya Abigail Chams kumshirikisha Harmonize katika wimbo wake, Me Too (2025) alichaguliwa kuwania tuzo za BET Marekani akiweka rekodi kama Msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kupata nafasi hiyo.
Video yake imetazamwa YouTube mara milioni 36.7, na hadi sasa hakuna video ya Abigail Chams iliyoweza hata kufikia nusu ya namba hizo, hivyo Harmonize anapofanya kolabo na msanii fulani mara kwa mara ujue tayari ameona matokeo makubwa mbele na ndivyo ilivyo na kwa Marioo.