Habari za michezo

OKELLO AWEKA REKODI, YANGA IKIREJEA KILELENI

Vardo May 22, 2026 10:27 pm

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Allan Okello, ameendelea kuonyesha umwamba wake kufuatia kufunga katika mchezo wa nne mfululizo wa Ligi Kuu Bara wakati timu hiyo ikirejea kileleni mwa msimamo baada ya jana kushushwa na Simba.

Katika mchezo huo uliochezwa leo Ijumaa Mei 22, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars, hivyo kufikisha pointi 57 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 55.

Okello aliwapa raha mashabiki wa Yanga dakika ya 13 ya mchezo huo, ikiwa ni rekodi kwa timu hiyo ya Wananchi ikiwa ni mchezaji pekee aliyefungua akaunti ya mabao katika mechi nne mfululizo.

Mganda huyo alifanya hivyo Mei 6, 2026 dhidi ya KMC wakati wakiisogeza timu hiyo shimoni kufuatia bao lake (1-0) kuifanya Yanga kuvuna pointi zote tatu muda mchache kabla ya kibarua cha kocha Pedro Goncalves kuota nyasi.

Katika mechi ya kwanza, Yanga ikiwa chini kaimu kocha mkuu Abdihamid Moallin, Okello alifunga mabao mawili na kutoa asisti moja dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Mei 13, licha ya Yanga kukumbana na kipigo cha kwanza (3-2) Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida, Okello alifunga mabao mawili ambayo hata hivyo hayakutosha kwa Wananchi.

Yanga ambayo ilikuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza kufuatia kufungwa katika mechi ya mwisho ya ligi, ilionekana kuwa na nguvu kubwa kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Baada ya Singida BS kuruhusu bao hilo la mapema, kocha wa kikosi hicho, Muhibu Kanu alifanya mabadiliko ya kwanza ambayo yalizua gumzo.

Katika dakika ya 23, alimtoa kipa Metacha Mnata ambaye hakuonekana kukubaliana na mabadiliko hayo na kuingia Amas Abasogie, ilibidi wachezaji wenzake kuongea naye kabla ya kutoka.

Hata hivyo, licha ya kufanywa kwa mabadiliko hayo, Singida BS iliruhusu bao la pili ambalo walifungwa dakika ya 41 na Mudathir Yahya na kufanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Yanga ilirejea kipindi cha pili na kufanya mabadiliko, alitolewa Pacome Zouzoua na kuingia Mohammed Damaro ili kuongeza nguvu eneo la kati ambalo Singida BS ilijaribu kulitumia kurudi mchezoni.

Singida BS nayo iliamua kumtoa Lamine Jarjou huku akiingia Chikola ili kuongeza nguvu maeneo ya pembeni hata hivyo Yanga ilionekana kuwa bora.

Katika dakika ya 62, Yanga ilifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Prince Dube na kuingia Depu. Wakati ambao Singida BS ikitafuta bao kurejea mchezoni, Okello alipiga msumari wa tatu.

Mabao hayo yamemfanya Okello kuwa na idadi sawa ya mabao na Prince Dube wote wakiwa na tisa, licha ya kutua Jangwani wakati wa dirisha dogo la Januari 2026, mbali na idadi hiyo ya mabao pia ametoa asisti saba.

Kwa mujibu wa takwimu, Okello ndiye mchezaji habari zaidi kwa Yanga huku akiweka rekodi ya kufunga mabao mawili ‘brace’ katika mechi tatu mfululizo za ligi. Hakuna mchezaji mwingine ambaye amefanya hivyo msimu huu.

Pia kuhusika kwake na mabao 16 akifunga tisa na asisti saba kwenye Ligi Kuu Bara akicheza kwa takribani miezi minne sasa, inampa nafasi ya kumuweka kwenye nyota hatari.

ELIUD AMBOKILE APATA MZUKA MPYA MBEYA CITY JANGWANI KUNA PESA, WAJANJA WANAICHUKUA FURSA SASA HIVI