MABAO matano aliyofunga straika wa Mbeya City, Eliud Ambokile, yameonekana kumwongezea morali, huku akiahidi kuipambania timu hiyo kuhakikisha inabaki salama Ligi Kuu Bara.
Mbeya City haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 22 na Mei 26, 2026 itakuwa uwanjani kuifuata Singida Black Stars katika mwendelezo wa Ligi Kuu ikisaka pointi tatu kujiweka pazuri.
Ambokile ambaye anaichezea timu hiyo kwa takribani misimu sita, msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa kwa kikosi hicho wakati kikishiriki Ligi ya Championship alipofunga mabao 16 yakiwamo matatu ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Nahodha huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa, licha ya matokeo waliyonayo kutoridhisha sana, bado wanaendelea kupambana kuhakikisha Mbeya City hairudi Championship huku akichekelea mabao matano aliyofikia kwa sasa.
Alikiri ligi kuwa ngumu kwa kila timu kupambania malengo yake na sare ya mechi iliyopita dhidi ya Namungo imewaongezea morali kikosini kuendeleza kasi hiyohiyo kwa michezo inayofuata.
“Nashukuru kwa idadi hii ambayo ni sehemu ya mwendelezo katika kupambania timu kupata matokeo mazuri, hatuko sehemu nzuri ila tunaamini tunaweza kufanya vizuri kwa mechi zilizobaki,” amesema nahodha huyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amesema baada ya pointi moja ugenini wanaendelea kukaza kuhakikisha mchezo dhidi ya Singida wanapata matokeo mazuri kuwaweka nafasi nzuri kwenye msimamo.
“Niwapongeze vijana kwa kuonyesha dhamira kuipambania timu, bado hatuko salama na tunahitaji matokeo mazuri kila mchezo ili kujiondoa kwenye presha ya kutoshuka daraja, haijaisha hadi iishe,” amesema Mayanga.