Habari za michezo
MARTINEZ NA MANDINHA NDANI YA PENZI LILILOANZIA STENDI LILILOMPA UBINGWA
Vardo
May 24, 2026
10:22 am
WIKI hii Aston Villa imeshinda ubingwa wa Europa League kwa kuichapa Freiburg mabao 3-0 gumzo kubwa baada ya mechi hiyo ni jinsi kipa Emiliano Martinez, 33, amekuwa akishinda fainali alizocheza ambazo zinafikia saba.
Hata hivyo, Martinez hakuwahi kushinda fainali yoyote kabla ya kufunga ndoa na mkewe, Amanda maarufu kama Mandinha, 39, hivyo baada ya kuanzisha familia tu, mambo yakaanza kumuendea vizuri baada ya changamoto nyingi alizopitia.
Martinez kutoka Argentina, akiidakia Aston Villa alishinda Kombe la FA 2020 dhidi ya waajiri wake zamani Arsenal, Ngao ya Jamii 2020 dhidi ya Liverpool na sasa Europa League 2026 dhidi ya Freiburg. Katika timu ya taifa alishinda fainali ya Copa America 2021 dhidi ya Brazil, Finalissima 2022 dhidi ya Italia, Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Ufaransa na Copa America 2024 dhidi ya Colombia.
Nyuma ya mafanikio hayo kuna na Amanda ambaye amekuwa pamoja na kipa huyo tangu 2013 baada ya kukutana jijini London wakati huo Martinez akiwa bado anajitafuta kimaisha na kisoka.
Kwa miaka zaidi ya 10, Mandinha amekuwa mmoja wa watu muhimu zaidi katika maisha yake akimtoa Martinez benchi hadi kuja kuwa kipa anayesifika duniani kwa kucheza vizuri karata zake linapokuja suala la fainali.
Kwa mujibu wa marafiki wa karibu, wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye stendi ya mabasi wakati huo Martinez akitafuta nafasi ya kudumu katika kikosi cha Arsenal, na punde tu uhusiano wao ukaanza. Walifunga ndoa mnamo Mei 2017 katika ukumbi wa kifahari wa Brocket Hall uliopo nje kidogo ya London, huku baadhi ya wachezaji wa zamani wa Arsenal wakihudhuria harusi hiyo.
Mwaka mmoja baadaye walimpata mtoto wao wa kwanza wa kiume, Santi, kisha mwaka 2021 wakapata wa pili wa kike ambaye wamempa jina la Ava. Akiwa kambini na timu ya taifa ya Argentina ndipo alipata habari kuwa Ava amezaliwa nchini Uingereza.
Kutokana na kuwa ndani ya mashindano huku Argentina akijiandaa kwa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Colombia, Martinez hakuweza kusafiri hivyo alimuona mtoto wake Ava kwa mara ya kwanza kupitia video call.
Siku chache baadaye, Martinez aliandika historia kwa kuonyesha kiwango bora zaidi katika mikwaju ya penalti dhidi ya Colombia katika mchezo huo, na kisha kuja kuisaidia Argentina kushinda taji hilo mbele ya Brazil.
Hivyo baada kufunga ndoa na Mandinha mwaka 2017 na kupata mtoto wao kwanza mwaka 2018, ulikuwa ni mwanzo mpya wenye neema nyingi katika soka la Martinez kwani kuazia hapo ameibuka shujaa katika fainali saba huku akitwaa tuzo ya Kipa Bora wa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Martinez kukutana na Mandinha na hatimaye kufikia mafanikio hayo kwani alipitia changamoto nyingi za kifamilia na kisoka. Martinez alikulia kwenye maisha ya umaskini mjini Mar del Plata nchini Argentina, baba yake Alberto alikuwa dereva wa malori aliyesafirisha samaki huku mama yake Susana akifanya kazi ya usafiri katika apartment.
Aliwahi kuelezea maumivu aliyokuwa nayo baada ya kumuona baba yake akilia usiku kutokana na kukabiliwa na madeni mengi, huku wazazi wake wakilala njaa ili kuhakikisha watoto wao wanapata chakula hata kama ni kidogo. Akiwa na umri wa miaka 12, Martinez aliondoka nyumbani na kwenda Buenos Aires kujiunga na akademi ya Independiente. Miaka mitano baadaye alipata nafasi ya kujiunga na Arsenal, na huku ndipo alipokuja kukutana na Mandinha.
Licha ya Arsenal kumpa mkataba mrefu lakini mambo hayakuwa rahisi kwake ndani ya klabu hiyo kwani hakupata namba hivyo kati ya mwaka 2012 hadi 2020 alitolewa kwa mkopo kwenda kwenye klabu sita tofauti. Ni kama maisha yake ya soka yalikuwa ya kutangatanga sana lakini baada ya Aston Villa kumnunua mwaka 2020, upepo ukabadilika na kuanza kutengeneza rekodi zake hizo.
Mkewe Mandinha aliyezaliwa Uingereza, mbali na kuwa mke wa golikipa maarufu duniani, yeye pia ana biashara zake na moja wapo ni kampuni ya Mi Suenos Kids inayojihusisha na mapambo na utengenezaji wa vyumba maalum vya watoto.Vilevile ni staa wa mitandao ya kijamii akiwa na wafuasi (followers) zaidi ya 734,000 Instagram ambapo kila mara huposti picha nyingi za familia yake wakisafiri kwa ndege binafsi au wakiwa uwanja kwenye mechi za mume wake. Kwa sasa Martinez kajipata kisoka na kimaisha, yeye na mkewe pamoja na watoto wao wawili wanaishi kwenye nyumba ya kifahari yenye thamani ya Pauni 2.3 milioni(takriban Sh8.2 bilioni).