LONDON, ENGLAND: KOMBE la Dunia ni mashindano makubwa zaidi ya soka duniani, na kwa miaka mingi yamekuwa kama jukwaa la kuzaliwa kwa nyota wakubwa wa mchezo huo duniani.
Wakati wachezaji wengi huhitaji muda na uzoefu mkubwa ili kung’ara katika kiwango hicho, baadhi ya vipaji vya kipekee vilifanikiwa kuweka historia vikiwa bado na umri mdogo sana.
Katika historia ya Kombe la Dunia, kumekuwapo na vijana wachache waliofunga mabao wakiwa wadogo, lakini hakuna aliyefanya hivyo kwa ubora na umaarufu mkubwa kama Edson Arantes do Nascimento maarufu Pele aliyekuja kuwa staa mkubwa Brazil na duniani. Hata hivyo, wengine kama Manuel Rosas, Gavi, Michael Owen na Nicolae Kovacs pia waliandika historia zao.
PELE (miaka 17 na siku 239)
Ilikuwa katika mechi kati ya Brazil dhidi ya Wales iliyopigwa Juni 19, 1958, Pele akiwa ndiye mchezaji mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika Kombe la Dunia alifanya vitu vyake. Akiwa na umri wa miaka 17 na siku 239, nyota huyo aliifungia timu yake bao muhimu katika robo fainali.
Bao hilo halikuwa tu rekodi kutoka kwa staa mwenye umri mdogo, bali lilikuwa mwanzo wa safari ya kihistoria iliyobadilisha soka duniani.
Pele alikuwa hajafikisha miaka 18, lakini tayari alikuwa anaonyesha uwezo uliowashangaza mashabiki na wachambuzi wa soka duniani kote. Katika mashindano ya 1958, alifunga jumla ya mabao sita, jambo ambalo hadi leo halijawahi kurudiwa na mchezaji mwingine yeyote. Katika nusu fainali dhidi ya Ufaransa, Pele alifunga hat-trick ya kihistoria na kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja wa Kombe la Dunia. Kana kwamba hiyo haitoshi, alifunga mabao mawili zaidi katika ushindi wa 5-2 dhidi ya Sweden kwenye fainali, na kuisaidia Brazil kutwaa Kombe la kwanza la Dunia. Pele pia anabaki kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga katika fainali ya Kombe la Dunia akiwa na miaka 17 na siku 249.
MANUEL ROSAS (miaka 18 na siku 93)
Beki huyo wa kimataifa wa Mexico ndiye mfungaji wa pili mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Kombe la Dunia alipotua dhidi ya Argentina iliyopigwa Julai 19, 1930. Katika mchezo huo, Rosas alifunga mabao mawili akiwa na umri wa miaka 18 na siku 93.
Lakini, kilichofanya jina lake liwe maarufu zaidi ni kwamba siku tatu kabla ya hapo, akiwa na miaka 18 na siku 90 alijifunga mwenyewe dhidi ya Chile. Bao hilo lilikuwa bao la kwanza la kujifunga katika historia ya Kombe la Dunia.
Pia, penalti aliyofunga dhidi ya Argentina ilikuwa penalti ya kwanza kufungwa katika historia ya mashindano hayo. Kwa maana hiyo, Manuel Rosas anabeba sehemu muhimu ya historia ya mwanzo wa Kombe la Dunia.
GAVI (miaka 18 na siku 110)
Katika Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, nyota chipukizi wa Hispania, Pablo MartÃn Paez Gavira maarufu Gavi aliweka historia kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuichezea nchi hiyo kwenye Kombe la Dunia na pia kufunga bao kwenye tukio la Novemba 23, 2022.
Katika ushindi mkubwa wa mabao 7-0 dhidi ya Costa Rica, Gavi alifunga bao la kuvutia kutoka nje ya eneo la hatari na kwa kufanya hivyo akawa mfungaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Kombe la Dunia na Mzungu mdogo zaidi kuwahi kufunga katika mashindano hayo. Mchezo huo pia uliingia kwenye rekodi kwa Hispania kuwa na umiliki mkubwa wa mpira na pasi nyingi zilizofanikiwa ndani ya dakika 90.
MICHAEL OWEN (Miaka 18 na siku 190)
Michael Owen alikuwa mojawapo wa vipaji vikubwa kabisa vya soka England mwishoni mwa miaka ya 1990 na katika gemu dhidi ya Romania iliyopigwa Juni 22, 1998 alifanya yake.
Katika Kombe hilo la Dunia nchini Ufaransa, nyota huyo alifunga bao lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 18 na siku 190 dhidi ya Romania, na baadaye alifunga bao moja maarufu sana dhidi ya Argentina kwenye hatua ya 16 bora ambalo hadi leo linatajwa kama mojawapo wa mabao bora zaidi katika historia ya England kwenye mashindano hayo.
Kwa miaka 24, Owen alikuwa Mzungu mdogo zaidi kufunga katika Kombe la Dunia hadi rekodi hiyo ilipovunjwa na Gavi 2022.
NICOLAE KOVACS (miaka 18 na siku 197)
Mromania Nicolae Kovacs alifunga bao lake pekee la Kombe la Dunia katika ushindi wa Romania wa 3-1 dhidi ya Peru Julai 14, 1930. Katika mchezo huohuo, mwenzake Constantin Stanciu pia alifunga akiwa na umri mdogo. Hadi leo, huo ndio mchezo pekee katika historia ya Kombe la Dunia ambapo vijana wawili wenye umri chini ya miaka 20 walifunga katika mechi moja.
Zipo pia rekodi za mastaa wadogo zaidi waliofunga mabao matatu katika mchezo mmoja zikiongozwa na Pele, ambaye mbali na kuwa mfungaji mdogo zaidi, pia ndiye mchezaji mdogo zaidi kufunga hat-trick katika Kombe la Dunia.
Nyota huyo alitengeneza rekodi hiyo 1958 dhidi ya Ufaransa akiwa na miaka 17 na siku 244. Hakuna mchezaji mwingine mwenye umri chini ya miaka 19 aliyewahi kufanya hivyo katika historia ya mashindano hayo.
Baada ya Pele, nyota mwingine pekee aliyewahi kufunga hat – trick ilikuwa katika fainali ya Kombe la Dunia ambaye ni Mbappe, aliyefanya hivyo dhidi ya Croatia katika fainali ya 2018 nchini Russia. Akiwa na miaka 19 na siku 207 aliisaidia Ufaransa kushinda mabao 4-2 na kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia.