news
WEMBANYAMA ALINGANISHWA NA GIANNIS KUVUNJA SHERIA NBA
Vardo
May 24, 2026
10:09 am
CALIFORNIA, MAREKANI: WAKATI San Antonio Spurs ikipigania nafasi ya kutinga fainali ya Ukanda wa Magharibi, nyota wake Victor Wembanyama ameibua mjadala mpya ndani ya ligi ya mpira wa kikapu ya NBA.
Wembanyama ambaye alikuwa moto wa kuotea mbali katika mchezo wa kwanza baada ya kufunga pointi 41 na kuokota rebound 24, aliisaidia Spurs kuanza vizuri mfululizo huo kwa ushindi muhimu dhidi ya Thunder ambao walikuwa hawajapoteza mchezo wowote katika hatua ya mchujo kabla ya hapo.
Kutokana na kiwango hicho, nyota huyo mwenye kimo kinachokaribia futi nane ameweka rekodi kadhaa mpya ndani ya NBA. Wembanyama sasa amekuwa mchezaji wa pili mwenye umri wa miaka 22 au chini kufikisha zaidi ya pointi 40 na rebound 20 katika mchezo wa mchujo, akimfuata nguli Kareem Abdul-Jabbar aliyefanya hivyo mwaka 1970.
Pia amejiunga na Shaquille O’Neal kama miongoni mwa wachezaji wachache waliofunga pointi 40 pamoja na rebound 20 katika mchezo wa kanda ndani ya miaka 25 iliyopita.
Hata hivyo, pamoja na sifa hizo, mjadala mkubwa umehamia kwenye namna anavyopiga mitupio ya adhabu. Mchambuzi maarufu wa NBC, Reggie Miller, amesema Wembanyama anaweza kuwa anakaribia kuvunja sheria za NBA kutokana na kutumia muda mrefu kabla ya mtupo wake wa adhabu.
Kwa mujibu wa sheria ya NBA Rule 9, kipengele cha kwanza, mchezaji anatakiwa kuachia mpira ndani ya sekunde 10 baada ya kupewa na mwamuzi. Miller alisema kila mara Wembanyama anapokwenda kwenye mstari wa adhabu, muda wake huwa uko karibu sana na sekunde hizo 10.
“Mahali fulani Giannis Antetokounmpo anasema, subiri kidogo! Kila mtupio wa adhabu wa Wemby uko karibu mno na sekunde 10,” alisema Miller.
Kauli hiyo imezua kumbukumbu za Giannis ambaye aliwahi kuingia matatani kutokana na kutumia muda mrefu kupiga mitupio ya adhabu. Katika mchujo wa mwaka 2021 dhidi ya Brooklyn Nets, mashabiki wa Nets walikuwa wakihesabu sekunde kwa sauti kila Giannis alipokuwa kwenye mstari wa adhabu huku akipata adhabu ya ‘10-second violation’€ mara kadhaa.
Katika mchezo huo dhidi ya Thunder, Wembanyama alipata pointi 13 kati ya 41 kupitia mipira ya adhabu, jambo lililoonyesha namna mbinu yake hiyo ilivyokuwa na mafanikio licha ya kuibua mjadala.
Licha ya ubora wao, Spurs bado wanaonekana kuwa timu changa yenye kiu ya kujifunza. Huu ni msimu wao wa kwanza kufika hatua ya mchujo tangu mwaka 2020, lakini Wembanyama amesema hawana hofu na changamoto zilizopo mbele yao.
“Tunataka kushinda kila kitu na tuna nafasi hiyo kwa sababu watu waliopo ndani ya klabu wanajua namna ya kufanikisha hilo,
alisema Wembanyama baada ya mchezo huo. Nyota huyo pia alisisitiza kuwa timu yao inaendelea kujifunza kupitia kila mchezo huku wakitumia nguvu kubwa kuziba mapungufu ya uzoefu.
Kwa ushindi huo, Spurs sasa wameboresha rekodi yao dhidi ya Thunder msimu huu hadi ushindi wa michezo mitano kati ya sita, jambo linalowapa matumaini makubwa ya kutinga fainali ya NBA kwa mara nyingine.