Simba Yaipania Yanga: Yaweka Mkataba Mpya wa Libasse Gueye Mezani Mpaka 2029!
Uongozi wa Simba SC umeanza mchakato wa haraka wa kumwongezea mkataba mpya kiungo mshambuliaji wake raia wa Senegal, Libasse Gueye, ili kuziba mianya yote inayoweza kutumiwa na klabu nyingine zikiwemo za ndani na nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kiwango bora na chenye muendelezo kinachoonyeshwa na mchezaji huyo msimu huu, hali iliyoanza kuvuta hisia za klabu mbalimbali, ikiwemo mpinzani wao mkubwa wa jadi, Yanga SC, ambayo inatajwa kufuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Gueye amekuwa nguzo muhimu katika eneo la ushambuliaji la Msimbazi, jambo lililowasukuma mabosi wa klabu hiyo kuchukua hatua mapema kabla ya mambo kuwa magumu.
Mkataba wa Sasa na Mipango ya Baadaye
Libasse Gueye alijiunga na Simba SC mnamo Januari 17, 2026, akitokea Teungueth FC ya Senegal, na kusaini mkataba wa miaka miwili na nusu unaotarajiwa kumalizika Juni 30, 2028.
Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Msimbazi zinaeleza kuwa uongozi umeamua kuongeza mwaka mmoja zaidi, hatua inayolenga kumfanya kusalia klabuni hapo hadi mwaka 2029.
Sababu za Simba Kuchukua Hatua Mapema
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimefichua kuwa uamuzi huo umetokana na somo ambalo klabu hiyo ililipata huko nyuma kwa kusubiri hadi mikataba ya wachezaji muhimu ikaribie kuisha.
“Moja ya jambo kubwa lililokuwa linatuangusha huko nyuma ni kusubiri hadi dakika za mwisho kumpa mkataba mpya mchezaji. Hali hiyo ilikuwa inatuweka katika presha kubwa, hususani tunaposhindana na timu nyingine zinazotaka huduma zao,” kilieleza chanzo hicho.
Kwa sasa, Simba imedhamiria kulinda uwekezaji wake mapema na kuhakikisha wachezaji wanaoleta tofauti uwanjani wanabaki kuwa sehemu ya mipango ya muda mrefu ya klabu hiyo.