Simba SC
SIMBA WAIKALIA KOONI YANGA BAADA YA USHINDI DHIDI YA DODOMA JIJI
Vardo
May 24, 2026
8:25 pm
UKISIKIA adui yako muombee mabaya, basi ndivyo ilivyo kwa Simba SC baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC na kutinga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha alama 58, huku wakiishusha Yanga SC hadi nafasi ya pili yenye pointi 57.
Bao pekee la ushindi la Simba lilifungwa na Elie Mpanzu dakika ya 62, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Dodoma Jiji FC, Daniel Mgore, kufuatia kupangua penalti iliyopigwa na Clatous Chama katika mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.
Dakika ya 61, Simba walipata penalti baada ya kipa huyo wa Dodoma Jiji kumchezea rafu Mpanzu ndani ya eneo la hatari, mwamuzi akaamuru mkwaju wa penalti ambao awali uliokolewa kabla ya Mpanzu kuandika bao la ushindi.
Matokeo hayo yameifanya Simba kurejea kileleni kwa muda, huku macho na masikio yao yakielekezwa kwenye mchezo wa kesho wa Yanga dhidi ya Namungo FC.
Iwapo Yanga itapoteza pointi kwa kutoka sare au kufungwa, Simba itaendelea kubaki kileleni mwa msimamo. Hata hivyo, endapo Wananchi wataibuka na ushindi dhidi ya Namungo, watarejea tena usukani wa ligi kwa kufikisha alama 60 na kuishusha Simba nafasi ya pili yenye pointi 58.