Michezo Bongo

TRA, JKT ZASHIKWA PABAYA, SINGIDA BS KICHEKO

Vardo May 24, 2026 8:45 pm

Mbio za kuwania nafasi ya nne imezidi kuwa wazi baada ya JKT Tanzania na TRA United kushindwa kupata ushindi katika michezo yao ya leo dhidi ya Mtibwa Sugar na Fountain Gate.

JKT Tanzania ilikubali kulazimishwa sare 2-2 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, na kufikisha pointi 38, huku TRA United (pointi 37) ikipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Fountain Gate.

Matokeo hayo ni habari njema kwa Singida Black Stars inayoshika nafasi ya nne ikiwa pointi 38 sawa na JKT lakini ikiwa mbele kwa tofauti ya mabao.

Singida BS baada ya kuchapwa na Yanga watashuka uwanjani Jumanne kuivaa Mbeya City iwapo watashinda watazidi kupaa katika mbio za kuwania nafasi ya nne.

Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wenyeji TRA United walipata kipigo cha kushtua kutoka kwa majirani zao Fountain Gate inayopambana kukwepa janga la kushuka daraja.

Wenyeji TRA United walioweka rekodi ya kutokufungwa uwanjani hapo na Yanga, Simba na Azam, hali ilikuwa tofauti leo baada ya kutangulia kwa bao la mapema lililofungwa na dakika ya 36, John Lazarus akimalizia pasi nzuri kutoka kwa Kassim Mgoya, lakini kabla ya bao hilo dakika ya 21, Ally Hamis Ng’anzi alifunga bao la mkono lililofutwa na mwamuzi Hery Sasii kisha kumpa adhabu ya kadi ya njano mchezaji.

Vijana na kocha Fred Minziro walipata bao la kusawazisha katika dakika ya 44, lililofungwa na kiungo mshambuliaji Ismail Azizi Kader akipokea pasi nzuri kutoka kwa Juma Abushiri aliyewapiga chenga mabeki wa TRA United kabla ya kutoa pasi hiyo.

Wakati mpira ukielekea mapumziko katika dakika mbili (dakika 45+) Kader alifunga bao la pili akiunganisha krosi ya  Chukwunonye Obasi ambaye ndiye kinara wa mabao nne katika kikosi hicho.

Kipindi cha pili Fountain Gate ilionekana kutawala mechi, huku TRA wakipambana kusawazisha na kocha  Etienne Ndayiragije alifanya mabadiliko dakika ya 77 alimtoa Mgoya na kumungiza mshambuliaji Shaaban Idd Chilunda ili kuongeza nguvu ya kushambulia.

Kocha wa Fountain Gate,Fred Felix Minziro alifanya mabadiliko dakika 83 walitoka S Sadick Ramadhan, Abushir, waliingia Elie Mokono, Shiga na mchezaji mwingine aliyetoka baada ya kuumia na kutolewa na machela nje Henry David akisindikizwa na kadi ya njano, aliyeingia kuchukua nafasi yake ni Shaban Mgunda.

Kocha Minziro aliyechukua mikoba ya aliyekuwa mtangulizi wake Mohamed Laizer, timu chini yake inaonekana kucheza kwa utulivu na mipango zaidi.

TRA iliyopo nafasi ya tano imeendelea kusalia katika nafasi hiyo, imecheza mechi 26, imeshinda 10, sare nane, imefungwa nane, inamiliki mabao ya kufunga 31 ya kufungwa mabao 24 ina pointi 37.

Wakati Fountain Gate iliyopo nafasi ya tisa licha ya kushinda mechi ya leo dhidi ya TRA United itaendelea kusalia nafasi hiyo isipokuwa zimeongezeka pointi kutoka 26 na sasa imefikisha alama 29, katika mechi  26, imeshinda nane, sare tano, imefungwa 12, inamiliki mabao 21 imefungwa mabao 36.

VINARA WA MABAO

TRA kina wa mabao ni Joseph Akandwanaho(mabao sita), Mapaka(mabao matatu),Chanda Chewe(mabao matatu),Ramadhan Salum Chobwedo(mabao matatu),

Fountain Gate ni Chukwunonye Obasi(mabao sita),Ismail Aziz,Sadick Ramadhani na Henry David kila mmoja amefunga mabao matatu.

MTIBWA YAIGOMEA JKT TANZANIA

Safu ya ulinzi wa JKT Tanzania watajilaumu kwa kushindwa kulinda ushindi wao dhidi Mtibwa Sugar baada ya kuongoza mara mbili kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mshambuliaji Paul Peter alifunga mabao mawili na kufikisha mabao nane katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu sambamba na Pacome Zouzoua wa Yanga, Mossi Nduwumwe wa Singida BS wote wamefunga mabao nane.

Peter alifunga mabao yake mawili katika dakika 19 na 43, wakati mabao ya kusawazisha ya Mtibwa Sugar yakifungwa na Haroun Lyawatwa dakika ya 36 akiunganisha mpira kwa kichwa uliopigigwa na kiungo nyota wa timu hiyo, Fredrick Magata kabla ya Magata kupachika bao la pili la kusawazisha katika dakika ya 68 kupitia mkwaju wa penalti baada ya nyota wa timu hiyo, Ismail Mhesa kufanyiwa madhambi eneo la 18 na beki waJKT Tanzania, Anuary Kilemile.

Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar imefikisha pointi 27 ikiwa nafasi 10, katika mbio zake za kukwepa kucheza hatua ya mtoano.

TIKETI YA TSH5 BILIONI KOMBE LA DUNIA, MHUDUMU INFANTINO