TEXAS, MAREKANI: MASHABIKI wa soka duniani wamepata afueni kidogo kuelekea Kombe la Dunia 2026 baada ya bei za tiketi kuanza kushuka katika soko la kuuza tena tiketi, lakini tiketi za mchezo wa fainali zikiwa ni dola milioni mbili (zaidi ya Sh 5.2 bilioni), kwa kwa siti za VVIP.
Rais wa FIFA, Gianni Infantino alizungumzia suala hilo mapema mwezi huu akisema kuwa kuwepo kwa tiketi zenye bei kubwa haimaanishi kuwa kuna watu wote watanunua kwa gharama hizo.
Infantino alisema mtu akinunua tiketi ya fainali kwa dola milioni mbili (zaidi ya Sh 5.2 bilioni), mimi binafsi nitakuhudumia kwa kuletea kitafunwa ‘hot dog’ na soda ili kuhakikisha anafurahia.
Kwa mujibu wa mtandao wa TicketData, unaofuatilia bei za tiketi zinazouzwa, wastani wa tiketi za hatua ya makundi umeshuka hadi dola 550 (zaidi ya Sh 1.4milioni) katika wiki ya mwisho. Hii ni tofauti na mwezi Aprili ambapo bei zilipanda hadi zaidi ya dola 700 (zaidi ya sh 1.8 milioni).
Hata hivyo, mashabiki wanaotaka kushuhudia mechi kubwa bado wanapaswa kujiandaa kutumia fedha nyingi. Mechi ya hatua ya makundi kati ya timu za taifa za Colombia na Ureno inayotarajiwa kuchezwa Florida Juni 27 imekuwa moja ya mechi zenye gharama kubwa zaidi huku tiketi ya chini kabisa ikitajwa kuuzwa kwa zaidi ya dola 2,500 (zaidi ya Sh6.5 milioni).
Mechi hiyo imezidi hata baadhi ya mechi za nusu fainali ambazo tiketi zake nyingi zinauzwa chini ya dola 2,300 ( zaidi ya Sh 6 milioni).
Kwa upande mwingine, baadhi ya michezo bado ina bei nafuu kwa mashabiki. Tiketi za mechi kati ya Austria dhidi ya Jordan huko Santa Clara, California, pamoja na mchezo wa Bosnia & Herzegovina dhidi ya Qatar mjini Seattle, zinaweza kupatikana kwa takribani dola 200 (karibu Sh 520,000).
Fainali ya Kombe la Dunia itakayochezwa katika uwanja wa MetLife huko New Jersey ndiyo yenye tiketi ghali zaidi. Tiketi ya bei ya chini kabisa imevuka dola 8,000 (zaidi ya Sh 20.8 milioni ) huku baadhi ya wauzaji wakitangaza tiketi kwa mamia ya maelfu hadi mamilioni ya dola.
Mwezi uliopita, mashabiki waliona tiketi nne za fainali zikiwekwa kwenye mfumo rasmi wa kuuza tiketi wa FIFA kwa karibu dola 2.3milioni kila moja (zaidi ya Sh 5.9 bilioni).
Wakati huo huo, meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, ametangaza kuwa wakazi wa jiji hilo watapata nafasi ya kununua tiketi 1,000 kwa dola 50 pekee (takribani Sh 130,000) kupitia mfumo wa bahati nasibu utakaoanza leo, Jumatatu. Tiketi hizo zitajumuisha pia usafiri wa bure wa basi kwenda uwanjani.
Bei za tiketi zimeendelea kuzua mjadala mkubwa nchini Marekani huku baadhi ya viongozi wa kisiasa wakitaka FIFA kutoa maelezo kuhusu mfumo wake wa upangaji bei.
Hata Rais wa Marekani, Donald Trump, alikosoa gharama hizo akisema kuwa hata yeye asingelipa maelfu ya dola kununua tiketi ya mechi.
Licha ya malalamiko hayo, FIFA imeendelea kusisitiza kuwa bei hizo zinaendana na viwango vya soko la burudani nchini Marekani na kwamba kuuza tena tiketi kunachangia kupanda kwa gharama kwa mashabiki.