Nahodha wa klabu ya Real Madrid, Dani Carvajal, ametangaza kuondoka kwenye klabu hiyo baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili tofauti ndani ya miaka 23.
Carvajal mwenye umri wa miaka 34 ameichezea Madrid mechi 450 na kufunga mabao 14. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Juni, hivyo ataondoka kama mchezaji huru.
Beki huyo wa kulia aliyezaliwa Madrid anachukuliwa kuwa mmoja wa magwiji wa klabu hiyo na miongoni mwa wachezaji waliofanikiwa zaidi kihistoria, akiwa ametwaa mataji 27.
Carvajal alijiunga na akademi ya Madrid mwaka 2002 na kucheza mechi yake ya kwanza katika kikosi cha wakubwa mwaka 2013 baada ya msimu mmoja akiwa na Bayer Leverkusen, hatua iliyosababisha Madrid kutumia kipengele cha kumrejesha klabuni.
Katika kipindi chake akiwa na Los Blancos, alitwaa taji la UEFA Champions League mara sita, akiwa mmoja wa wachezaji watano pekee kufanikisha hilo, na ndiye mchezaji pekee aliyeanza katika fainali zote sita alizoshinda.
Pia alishinda mataji manne ya La Liga, mawili ya Copa del Rey, sita ya Kombe la Dunia la Klabu, matano ya UEFA Super Cup na manne ya Spanish Super Cup.
Kwa sasa mchezaji huyo anatajwa kuelekea kwenye kikosi cha Inter Miami cha Marekani ambao wameshafanya naye mazungumzo, lakini kukiwa pia na uwezekano wa kujiunga na Inter Milan.
Rafael Leao
AC Milan wako tayari kumuuza winga wa Ureno, Rafael Leao, kwa ada ya chini huku Manchester United wakitajwa kuonyesha nia ya kumsajili.
Leao mwenye umri wa miaka 26 anapatikana kwa ada ya pauni 43 milioni. Leao amekuwa akitajwa kama mmoja kati ya wachezaji mahiri kwenye kikosi hicho na inaaminika kuwa anaweza kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha United.
Valentin Barco
Chelsea wamekubaliana kumsajili beki wa kushoto wa zamani wa Brighton & Hove Albion, Valentin Barco, kutoka klabu ya Strasbourg.
Chelsea inapambana kuhakikisha kuwa inakuwa na kikosi imara ambacho kinaweza kuwania makombe msimu ujao kikiwa chini ya kocha mpya Xabi Alonso.
Msimu huu haijawa na kiwango bora na imejikuta ikishushwa kutoka nafasi ya nne hadi ya tisa kwenye msimamo na hivyo kuona kikosi kina shida.
Alisson Becker
Kipa wa Liverpool, Alisson Becker, yuko tayari kujiunga na Juventus na kuungana tena na kocha wake wa zamani wa Roma, Luciano Spalletti, huku akiwaniwa pia na AC Milan.
Tangu awali kipa huyo mwenye uzoefu wa hali ya juu alishasema kuwa anataka kujiunga na Juventus kwa kuwa ana marafiki wengi kwenye timu hiyo akiwemo kocha mkuu wa kikosi hicho. Msimu huu amecheza mechi 28 za ligi na ana cleansheet nane.
Thiago Silva
Chelsea wanataka beki wao wa zamani Thiago Silva kurejea klabuni kama kocha baada ya kuondoka Porto, lakini AC Milan wamempa ofa ya mkataba wa mwaka mmoja ili aendelee kucheza.
Thiago ni mmoja kati ya wachezaji ambao walifanya vizuri wakiwa na Chelsea na kuondoka kwenye kikosi hicho kwa heshima kubwa na hivyo wanataka arudi akasaidie kukibadili kikosi chao kiwe cha kushindania makombe.
Jakub Kiwior
Beki wa zamani wa Arsenal, Jakub Kiwior, ambaye sasa anachezea Porto, anafuatiliwa na Barcelona huku mabingwa hao wa La Liga wakiamini kuwa ni mmoja kati ya mabeki bora kwa sasa.
Arsenal iliachana na beki huyo baada ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, hata hivyo amefanikiwa kufanya mambo makubwa akiwa na Porto msimu uliopita na kuwashawishi mabosi wa Barca.
Arijon Ibrahimovic
Brighton & Hove Albion na Crystal Palace ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazomtaka kiungo wa Bayern Munich mwenye miaka 20, Arijon Ibrahimovic, baada ya kung’ara akiwa kwa mkopo Heidenheim.
Staa huyo amefanikiwa kuonyesha kiwango bora na kuziingiza timu hizo vitani, mbali na Brighton na Palace pia Everton imeonyesha nia ya kumtaka mchezaji huyo.
William Osula
Aston Villa wanavutiwa na mshambuliaji wa Denmark, William Osula, lakini Newcastle United wamesisitiza hawatamuuza baada ya kujihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza chini ya kocha Eddie Howe.
Osula alifanya vizuri akiwa na Newcastle msimu uliomalizika jana na sasa amekuwa akiziingiza vitani klabu kadhaa za ligi hiyo na mwenyewe amewahi kusema hana mpango wa kuondoka.