Yusuph Mhilu
Michezo Bongo

Yusuph Mhilu Apona Majeraha Geita Gold, Atuma Onyo Ligi Kuu Bara

Vardo September 26, 2026 8:02 pm

MSHAMBULIAJI nyota wa Geita Gold, Yusuph Mhilu, amerejea uwanjani rasmi baada ya kupona kabisa majeraha ya nyama za paja yaliyomweka nje kwa muda.

Mhilu alipata majeraha hayo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC uliyopigwa kwenye Uwanja wa Bukombe, mji mdogo wa Ushirombo mkoani Geita, Agosti 28, 2026. Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 2-2, ulimshuhudia mshambuliaji huyo akitoka uwanjani dakika ya 12 pekee baada ya kushindwa kuendelea.

Akizungumza kuhusu hali yake ya sasa, Mhilu amethibitisha kuwa yupo fiti kwa asilimia 100 na tayari anafanya mazoezi na wachezaji wenzake kuelekea mechi zijazo za Ligi Kuu Bara baada ya kumalizika kwa kalenda ya FIFA.

“Kwa sasa nimerejea katika hali yangu ya kawaida. Awali nilipata changamoto ya kurudia majeraha baada ya kufosi kucheza mapema, lakini baada ya hapo niliamua kutulia kwanza ili nipone vizuri. Hivi sasa niko tayari kwa mapambano,” alisema Mhilu.

Kurejea Kwake Kuongeza Machaguo Kikosini

Mhilu aliongeza kuwa kurejea kwake ni habari njema kwa benchi la ufundi la Geita Gold kwani kunapanua wigo wa machaguo katika idara ya ushambuliaji, ingawa anatambua uwepo wa ushindani mkali wa namba kutoka kwa wachezaji wengine kikosini.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu za Yanga, Simba na Ndanda FC, alijiunga na Geita Gold Julai 21, 2023, akitokea Kagera Sugar. Mpaka sasa, tayari ameshafumania nyavu mara mbili kwenye msimu huu wa 2026-2027.

Mhilu ni mfungaji wa pili wa muda kwenye kikosi cha Geita Gold, akimfuatia mshambuliaji Mzambia Obrey Chirwa mwenye mabao 4. Chirwa, ambaye pia amewahi kuzipitia timu za Yanga, Azam FC, Namungo FC, Singida Black Stars na KenGold, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Championship akiwa na mabao 18—sawa na mchezaji mwenzake wa Geita Gold, Maulid Shaaban.

Coastal Union Afichua Siri Baada ya Kukutana na Simba na Yanga Barker ana Puzzle ya Nyota 10: Kambi ya Simba Sauzi ina Sura Mbili Kabla ya Dabi