CHIRWA APANIA KUIPANDISHA KAGERA SUGAR
MSHAMBULIAJI wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa amesema licha ya kasi yake ya kufunga mabao msimu huu, ila kipaumbele chake cha kwanza ni kukirejesha kikosi hicho Ligi Kuu Bara, hata kama ikitokea pia akakosa tuzo ya ufungaji bora.
Akizungumza na Soka la Bongo, Chirwa amesema anachoangalia kwa sasa ni mafanikio ya timu hiyo kijumla na siyo yake binafsi, jambo ambalo ni kipaumbele cha kwanza kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa kikosi hicho.
“Niko katika nafasi nzuri ya kushinda tuzo ya mfungaji bora ikiwa nitaendelea kufanya vizuri katika mechi zilizobakia, hii inanipa hamasa lakini kipaumbele changu cha kwanza ni kuirudisha tena Kagera Ligi Kuu msimu ujao,” amesema Chirwa.
Chirwa sio jina geni kwa mashabiki na wadau wa soka hapa Tanzania, kutokana na wasifu wake tangu nyota huyo alipojiunga na Yanga kwa mara ya kwanza, Julai 1, 2016, akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na kuzidi kujizoelea umaarufu kila kukicha.
Baada ya kuichezea Yanga kuanzia Julai 1, 2016, aliachana nayo Julai 17, 2018, kisha kujiunga na Nogoom FC ya Misri, kabla ya kurejea tena nchini na kujiunga na Azam FC, Novemba 8, 2018, huku akiichezea pia, Hobro IK kutoka Denmark.
Nyota huyo aliziyechezea pia Namungo FC, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na KenGold, ameonyesha kiwango bora msimu huu akiwa na kikosi cha Kagera Sugar ambacho amekifungia mabao 16 na ndiye kinara wa mabao.
Kagera iliyodumu Ligi Kuu kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki mwaka 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025 na kwa sasa iko nafasi ya pili na pointi 62, baada ya kushinda mechi 19, sare tano na kupoteza mbili, ikifunga mabao 47 na kuruhusu 12.