SIMBA LENGO KUBEBA MATAJI, SI KUJALI MAJINA YA WAPINZANI
MWENYEKITI wa Simba SC, Murtaza Mangungu, ameweka wazi msimamo wa klabu hiyo kuelekea msimu huu, akisisitiza kuwa malengo yao makubwa bado ni yale yale—kushindana kwa kiwango cha juu na kuhakikisha mataji yanabaki Msimbazi.
Mangungu amesema Simba haichezi kwa kuangalia ukubwa au majina ya wapinzani, bali inalenga kujitathmini yenyewe na kuhakikisha kila mchezo unaleta matokeo chanya yanayowakaribisha kwenye mafanikio ya mwisho wa msimu.
Mangungu amesisitiza kuwa katika hatua hizi za lala salama za ligi, kila pointi ina thamani kubwa, hasa ikizingatiwa ushindani mkali unaoendelea kati ya timu tano za juu ambazo zote bado zina nafasi ya kuamua hatma ya ubingwa.
“Malengo yetu ni yale yale, kushindana na kuchukua mataji. Simba tumeshinda mechi zetu, hatuangalii wapinzani wetu. Hatutaki kutengeneza hofu kwa timu fulani,” amesema Mangungu.
Kauli hiyo inaashiria imani kubwa ndani ya uongozi wa Simba kuhusu mwenendo wa kikosi hicho, huku wakisisitiza kuwa nidhamu, uthabiti na umakini kwenye kila mchezo ndio silaha kuu katika mbio hizo za ubingwa.
Mashabiki wa Simba sasa wanaendelea kusubiri kuona kama timu yao itaendeleza makali hayo hadi mwisho wa msimu na kufanikisha lengo la kutwaa mataji kama ilivyokusudiwa.