OKELLO AONYWA PRESHA, KAMWE AMPIGIA DEBE FEI TOTO
MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe, ameibua mjadala mkubwa kuhusu mbio za tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara (MVP) msimu wa 2025/26, baada ya kuweka wazi kuwa kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ndiye anayeonekana kuwa mbele zaidi katika kuwania tuzo hiyo kwa sasa.
Kamwe amesema kiwango anachoendelea kukionyesha Fei Toto ndani ya uwanja ni cha kipekee, hasa kutokana na mchango wake mkubwa kwenye mabao na ubunifu wa mashambulizi kwa timu yake msimu huu.
Kwa mujibu wa Kamwe, nyota huyo wa Azam FC ameonyesha ubora wa hali ya juu kupitia uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao, jambo linalomfanya kuwa na nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka nchini.
Mbali na kumzungumzia Fei Toto, Kamwe pia alitoa kauli kuhusu kiungo wa Yanga SC, Allan Okello, ambaye naye ametajwa mara kadhaa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania MVP kutokana na kiwango chake bora msimu huu.
Hata hivyo, Kamwe aliwataka mashabiki wa Yanga kutomwekea presha Okello kwa mjadala wa tuzo binafsi, akisisitiza kuwa jambo muhimu kwa sasa ni nyota huyo kuendelea kuitumikia timu yake ipasavyo na kusaidia Yanga kufikia malengo yake ya msimu.
“Tusimpe presha Okello kuhusu mchezaji bora wa msimu. Muacheni afanye majukumu yake uwanjani. Hata ligi ikimalizika leo, MVP anajulikana na ni Fei Toto kutokana na kile anachokifanya ndani ya timu yake na namna anavyoongoza kwenye mchango wa mabao,” amesema Kamwe.
Mpaka sasa, Fei Toto ameendelea kuwa kwenye kiwango bora akiwa tayari amefunga mabao 14 na kutoa asisti nane katika Ligi Kuu Bara, takwimu zinazomuweka miongoni mwa wachezaji wenye ushawishi mkubwa zaidi msimu huu.
Kwa upande wa Allan Okello, kiungo huyo wa Yanga naye ameendelea kuwa mhimili muhimu ndani ya kikosi hicho, akiwa amefunga mabao 11 na kutoa asisti saba, huku kiwango chake kizuri kikizidi kumuweka kwenye rada ya tuzo mbalimbali binafsi.
Kauli ya Kamwe imeongeza moto kwenye mjadala wa nani anayestahili kutwaa tuzo ya MVP msimu huu, huku mashabiki wa soka wakizidi kusubiri kuona nani ataibuka kidedea mwishoni mwa msimu.