BAO LA MPANZU LAIBUA GUMZO, AHMED ALLY AWEKA WAZI UKWELI
MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameibuka na kueleza kwa kina kilichoifanya bao la kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Elie Mpanzu, kuwa la kipekee katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji, baada ya bao hilo kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka.
Ahmed amesema wengi wameishia kuona namna Mpanzu alivyomalizia mpira wavuni, lakini hawakugundua kazi kubwa ya kiakili aliyofanya sekunde chache kabla ya bao hilo kuzaliwa.
Kwa mujibu wa Ahmed, kilichomtofautisha Mpanzu si nguvu wala bahati, bali ni uwezo wake mkubwa wa kusoma mchezo mapema na kufanya maamuzi ya haraka ndani ya muda mfupi.
Amefafanua kuwa wakati wachezaji wengi walikuwa bado wakisubiri kuona matokeo ya penalti, Mpanzu tayari alikuwa ameanza kukimbia kwa kasi kuelekea eneo hatari, akionesha anticipation ya hali ya juu.
“Watu wengi wameona Mpanzu akifunga, lakini hawakuona alianza lini kukimbia. Hapo ndipo tofauti yake ilipo,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa nyota huyo alionesha umakini mkubwa tangu mpigaji wa penalti alipoanza maandalizi ya kupiga mpira, kwani tayari alikuwa ameusoma mwelekeo wa tukio mapema kuliko wapinzani wengine waliokuwa bado wamesimama kusubiri kitakachotokea.
Ahmed amesema kitendo hicho kinaonyesha kiwango kikubwa cha akili ya mpira na activeness ambayo mara nyingi huwatofautisha wachezaji wa kawaida na wale wa kiwango cha juu.
“Hapa ndipo unaona akili ya mchezaji. Wengine walikuwa wamesimama wakisubiri matokeo ya penalti, lakini Mpanzu alikuwa tayari ameanza safari ya kwenda kumalizia,” ameongeza.
Mbali na kupongeza utulivu wake ndani ya eneo la hatari, Ahmed amelilinganisha bao hilo na yale yanayofungwa na mastaa wakubwa duniani, akisisitiza kuwa lilikuwa bao la kiwango cha juu lililobebwa na kasi, umakini na maamuzi sahihi ya haraka.
“Hili si bao la kawaida. Ni bao ambalo linaonyesha mchezaji mwenye akili ya mpira na utulivu mkubwa ndani ya eneo la hatari,” amesema Ahmed Ally.