HERSI AINGIZA YANGA KWENYE VITA KUBWA YA USAJILI AFRIKA
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameingia tena kwenye ukurasa mpya wa jitihada za usajili baada ya kuibuka na mpango mzito wa kumnasa kiungo mshambuliaji wa Al Hilal, Jean Claude Girumugisha, katika dirisha lijalo la usajili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo karibu na mazungumzo hayo, uongozi wa Yanga unatarajiwa kukutana tena na mwenyekiti wa Al Hilal, Hesham Hassan Al-Subat, kwa lengo la kufungua upya mazungumzo yaliyokwama awali na kuona kama kuna uwezekano wa kufanikisha dili hilo ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa karibu.
Katika mkutano wa awali kati ya pande hizo mbili, changamoto kubwa ilitajwa kuwa ni kipengele cha release clause kwenye mkataba wa mchezaji huyo, ambacho kilifanya mazungumzo hayo kugonga mwamba licha ya nia ya Yanga kuendelea kusukuma mbele dili hilo.
Hata hivyo, Yanga hawajakata tamaa.
Kwa kushirikiana na mdhamini wao mkuu GSM, klabu hiyo imeandaa ofa mpya ya kiasi cha Shilingi Bilioni 1.5, ikiwa ni mkakati wa kumshawishi Al Hilal kukubali kumuachia nyota huyo.
Rais wa Yanga, Hersi Said, anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mazungumzo hayo ya pili yatakayofanyika muda wowote kuanzia sasa, akiwa na dhamira ya kuona dili hilo linafika tamati na Yanga inapata huduma ya mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa eneo la ushambuliaji.
Kwa upande mwingine, taarifa zinaeleza kuwa hata baadhi ya wadau wakubwa wa Al Hilal, akiwemo mfadhili maarufu Turki Al-Sheikh, bado hawajaonyesha mwelekeo wa kuunga mkono uuzwaji wa mchezaji huyo kutokana na umuhimu wake ndani ya kikosi.
Hata hivyo, upande wa Yanga unaendelea kuwa na matumaini makubwa, hasa baada ya mazungumzo ya awali kati ya klabu na mchezaji mwenyewe kuonyesha dalili chanya, hali inayoongeza presha kwa Al Hilal kufanya uamuzi mgumu.
Malengo ya mabingwa hao ni kukamilisha dili hilo kabla ya wiki ya pili ya mwezi Septemba, wakiamini kuwa usajili huo unaweza kuwa nyongeza muhimu katika kampeni zao za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa msimu ujao.