Michezo Bongo

LIGI KUU NBC KUREJEA JUNE,12 VITA VYA UBINGWA KUANZA UPYA

Vardo May 26, 2026 1:33 pm

BAADA ya michezo ya leo ya Ligi Kuu
Tanzania Bara ambapo Singida Black Stars watavaana na Mbeya City, huku Pamba Jiji wakipambana na Tanzania Prisons, ligi itaingia kwenye mapumziko mafupi kabla ya kurejea kwa kasi mpya ya ushindani.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza ratiba mpya ya kumalizia msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2025/2026 pamoja na fainali ya Kombe la CRDB Cup, hatua inayoongeza msisimko zaidi kwa mashabiki wa soka nchini.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Ligi Kuu itarejea rasmi Juni 12, 2026, baada ya mapumziko mafupi yatakayopisha kalenda ya mechi za kimataifa za FIFA.

Baada ya kurejea kwa ligi, kila timu itakuwa na mechi tano pekee za kumalizia msimu. Hapo ndipo mtihani halisi unapozidi kuwa mzito, kila pointi sasa ina thamani ya dhahabu, na makosa yanakuwa hayana nafasi tena.

Vita ya ubingwa, nafasi za kushiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na vita ya kubaki ligi kuu, vyote vinaingia kwenye hatua ya maamuzi makali.

Timu zote zitalazimika kucheza kwa akili, nguvu na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia malengo yao.
Lakini msimu hautaishia kwenye Ligi Kuu pekee.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo hiyo, fainali ya Kombe la CRDB Cup itapigwa Julai 4, 2026, ambapo bingwa atatawazwa rasmi na kufunga pazia la msimu mzima wa 2025/2026.

Sasa macho yote yanaelekezwa uwanjani—kila timu ikipigania historia yake, kila mchezo ukiwa ni fainali ndani ya fainali. Mbio za ubingwa na vita ya CRDB Cup zimeingia katika moto wa mwisho kabisa.

HERSI AINGIZA YANGA KWENYE VITA KUBWA YA USAJILI AFRIKA SIMA SC YACHACHAMAA, AHMED ALLY ASEMA MAPUMZIKO NI FURSA YA KUIMARIKA VITA VYA UBINGWA