SIMA SC YACHACHAMAA, AHMED ALLY ASEMA MAPUMZIKO NI FURSA YA KUIMARIKA VITA VYA UBINGWA
KATIKA kile kinachoendelea kuwa moja ya misimu yenye ushindani mkali zaidi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, upande wa Simba SC unaonekana kutotetereka hata kidogo licha ya kuwepo kwa mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema hali ya ligi msimu huu imekuwa ngumu na ya ushindani mkubwa, lakini ndani ya kikosi chao bado mambo yanaendelea kama kawaida ya “vita ya ubingwa.”
Kwa mujibu wake, hata katika kipindi hiki cha mapumziko mafupi, Simba haioni kama imepumzika kihalisi, kwani timu inaendelea na programu maalum zilizoandaliwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Steve Barker.
“Katika haya mapumziko ya FIFA kuna mapumziko mafupi, lakini kwetu ni kama hakuna mapumziko kwa sababu kila mchezaji anatakiwa kujifua na kuwa fiti kwa ajili ya ligi inaporejea. Tunaendelea tulipoishia,” amesema Ahmed .
Ameongeza kuwa ushindani wa ligi umefikia kiwango kikubwa, lakini Simba inabaki na malengo yake bila kuyumba, huku ikilenga kufanya vizuri katika michezo mitano iliyosalia bila kujali ukubwa wa wapinzani wao.
Kauli hiyo inaonyesha wazi kuwa Simba SC inaingia kwenye hatua ya mwisho ya msimu ikiwa imejipanga kikamilifu, huku macho yote yakielekezwa kwenye mbio za ubingwa zinazozidi kupamba moto.