MGUNDA AKIRI PRESHA MATOKEO MABOVU
KOCHA wa Namungo FC, Juma Mgunda amesema matokeo ambayo wamekuwa wakiyapata yamewaweka kwenye presha kubwa kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Tangu Januari 31, ilipokutana na KMC na kushinda bao 1-0, Namungo haijavuna alama tatu, zaidi ya kupoteza au sare, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kuporomoka hadi nafasi ya 13 ikiwa na pointi 25.
Mgunda alisema kucheza mechi 14 za Ligi bila ushindi ni hali ngumu kwake na wachezaji wake, licha ya kuwa wakionyesha kiwango kizuri uwanjani. “Matokeo ambayo tumeyapata hadi sasa yanatulazimisha kuwa kwenye presha kubwa kwa sababu timu haifanyi vizuri,” alisema Mgunda. “Kucheza mechi 14 za Ligi bila ushindi ni hatua ngumu kwetu kwa kuwa tunacheza vizuri, lakini tunakosa matokeo.”
Mgunda alisema bado hawajakata tamaa kwani wanaamini hali inaweza kubadilika mara watakapopata ushindi ambao utawarejeshea hali ya kujiamini.
“Hatutaki kukata tamaa. Tunaamini mambo yatabadilika tukishinda hata mchezo mmoja tu, itaturudishia hali ya kujiamini kwani bado tuna mechi tano mkononi, hivyo ni suala la kufanya mabadiliko ya haraka,”.
Kocha huyo alisema anaendelea kujipanga kupunguza makosa ambayo yamekuwa yakiigharimu timu hiyo.
“Mabao mengi ambayo tunaruhusu yanatokana na makosa yetu wenyewe, hivyo tunajipanga kuhakikisha tunapunguza makosa hayo,” alisema Mgunda.