SABABU YA LINGARD KUITWA JLINGZ YAFICHUKA
SANTOS, BRAZIL: SABABU ya kiungo Jesse Lingard kutumia jina la “JLingz” mgongoni mwa jezi yake imefichuka baada ya Corinthians kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Barra katika michuano ya Copa do Brasil.
Lingard, ambaye aliwahi kuitumikia Manchester United, alijiunga na Corinthians mwezi Machi mwaka huu baada ya kuondoka FC Seoul ya Korea Kusini mwishoni mwa mwaka 2025.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 alianza maisha mapya Brazil licha ya kuhitajika na klabu kadhaa zikiwemo West Ham United na Wolves.
Mwanzo wake Corinthians umekuwa wa kupanda na kushuka huku timu hiyo ikiwa nafasi ya 16 kwenye ligi baada ya michezo 15, lakini imeonyesha kiwango kizuri katika Copa Libertadores kwa kushinda michezo mitatu kati ya minne ya kwanza.
Lingard alianza mchezo wa marudiano dhidi ya Barra ambapo Corinthians ilitinga hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 2-0 baada ya nyota huyo kufunga bao la ushindi katika mchezo wa kwanza.
Mashabiki wengi walishangazwa kuona jezi yake ikiwa na jina “JLingz” badala ya Lingard, lakini hatua hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni maalum nchini Brazil kuadhimisha Siku ya Dawa Generic.
Wachezaji wote wa Corinthians walivaa majina yao ya utani mgongoni mwa jezi ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuonyesha umuhimu wa dawa Generic katika sekta ya afya ya umma nchini humo.
Sheria ya dawa generic nchini Brazil ilianzishwa Mei 20, 1999 na kusaidia wananchi kupata dawa bora kwa gharama nafuu zaidi.
Katika taarifa yao, Corinthians walieleza kuwa kampeni hiyo ilikuwa na ujumbe kwamba “jina linaweza kuwa tofauti lakini athari yake ni ile ile.”
Lingard pia aliandika historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Uingereza kufunga bao katika michuano ya Copa do Brasil baada ya kufunga bao hilo muhimu dhidi ya Barra mwezi uliopita.