RATIBA LIGI KUU BARA YAWAGAWA WADAU
KITENDO cha Ligi Kuu Bara kumalizika Juni 30, 2026 badala ya Mei 2026 kama ilivyopangwa awali, kimeibua mjadala mkubwa kwa wadau wa soka nchini.
Wapo wanaoona mabadiliko hayo yanaweza kuwaathiri wachezaji, wengine wakiamini yatawapa nafasi ya kupumzika baada ya mechi nyingi mfululizo.
Soka la Bongo limezungumza na mastaa mbalimbali wa zamani ambao kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa waandaaji wa ratiba kuhakikisha msimu unamalizika ndani ya muda uliopangwa, badala ya kusogezwa mbele mara kwa mara.
Beki wa zamani wa Simba, Frank Kasanga ‘Bwalya’, alisema kuchelewa kumalizika kwa ligi kunaweza kuwaathiri wachezaji, hasa wale wanaotafuta dili za usajili wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, alisema kama msimu wa 2026-2027 utaanza muda mfupi baada ya wa sasa kumalizika, hali hiyo inaweza kusababisha uchovu mkubwa kwa wachezaji.
Mbali na hilo, Bwalya alisema kusimama kwa ligi kupisha kalenda ya FIFA kunaweza kushusha morali na viwango vya baadhi ya wachezaji, hususan kama hawatakuwa kambini kuendelea na mazoezi.
“Nimekuwa mchezaji, najua wachezaji wanakuwa na mambo mengi. Wakikaa nyumbani kwa wiki mbili bila programu maalumu ni rahisi kushusha viwango. Ni vyema wakaendelea kuwa kambini na kufanya mazoezi chini ya makocha wao. Mchezaji kusajiliwa kwa fedha nyingi kunatokana na kiwango chake kuwa juu. Wapo wanaofuatiliwa na timu za ndani na nje, hivyo wakirejea kucheza mechi zilizobaki wakiwa chini ya kiwango, wanaweza kujikosesha nafasi za kupata mikataba mizuri,” alisema.
Kwa upande wake, staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni sehemu ya benchi la ufundi la Fountain Gate, Henry Joseph Shindika, alisema ni vigumu kutoa hukumu kamili kuhusu kuchelewa kwa ligi bila kujua tarehe rasmi ya kuanza kwa msimu mpya.
“Kwa mfano, mchezaji wa kikosi cha kwanza anayehitajika na timu ya nje atalazimika kwanza kuzungumza na viongozi wa klabu yake. Katika mechi tano zilizobaki anaweza asiwe na jipya kubwa la kuonyesha, lakini changamoto inakuja kama timu yake bado inamhitaji sana. Hapo inakuwa vigumu kwake kufanikisha dili kwa haraka kwa kuwa sasa kila timu ina kitu inawania, hii itawafanya wengi wakose madili,” alisema.