MESSI WA CHUGA ANUKIA ULAYA
UONGOZI wa Fountain Gate FC umepokea barua kutoka timu mbalimbali Ulaya ili kumpata kiungo mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Juma Issa Abushiri ‘Messi wa Chuga’ kwa lengo la kwenda kufanya majaribio msimu wa 2025-2026, utakapoisha.
Akizungumza na Soka la Bongo, Rais wa Fountain Gate, Japhet Makau alisema yapo mazungumzo na timu mbalimbali kutokea Ulaya ambazo zimeonyesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo kwa ajili ya majaribio, ingawa ni mapema kuzungumzia hilo.
“Ni kweli mazungumzo hayo yapo na sio Abushiri pekee, wapo na wengine, malengo yetu sisi Fountain Gate ni kuona vijana wenye vipaji wanapiga hatua kubwa na kukuza karia zao katika maisha hasa kwa kuwatoa nje ya nchi,” alisema Makau.
Aidha, Makau alisema suala la mchezaji huyo lipo hatua za mwisho kukamilika kwa sababu zipo nchi zaidi ya tatu za Ulaya ambazo zinamhitaji kwa ajili ya majaribio, hivyo mchakato huo bado unaendelea na pindi utakapokamilika watauweka wazi.
Miongoni mwa timu zinazomhitaji mchezaji huyo ni SK Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech, Malmo FF ya Sweden, Como 1907 ya Italia na moja ya England ambayo haijawekwa wazi na hadi sasa mazungumzo yanaendelea na uongozi wa Fountain Gate.
Abushiri mwenye mabao mawili ya Ligi Kuu Bara msimu huu wa 2025-2026 akiwa na kikosi cha Fountain Gate, ni miongoni mwa vijana wenye vipaji vikubwa na kwa sasa amegeuka lulu sokoni kutokana na kiwango bora anachoendelea kukionyesha.
Nyota huyo alianza kupata mafunzo ya soka katika Kituo cha Future Star kilichopo jijini Arusha, kisha uongozi wa Shule za Fountain Gate ukampa ufadhili wa kimasomo kutokana na mpira, jambo ambalo limemsaidia hadi sasa.