Ni Nafasi Nyingine Kwa Jonathan Sowah
JONATHAN Sowah kwa taarifa tulizonazo hapa kijiweni ni kwamba anarudi nchini kujiunga na Singida Black Stars.
Kwanza kijiwe kinakiri wazi kwamba Jonathan Sowah ni miongoni mwa washambuliaji wazuri ambao wamebahatika kucheza katika Ligi yetu siku za hivi karibuni.
Anajua kufunga na ni aina fulani ya mshambuliaji ambaye anapokuwepo uwanjani, mabeki na makipa wa timu pinzani huwa wanapoteza amani na utulivu wao.
Changamoto kubwa ambayo inaonekana kumuumiza Sowah ni ya nje ya uwanja jambo linalomfanya asiwe anadumu katika timu mbalimbali ambazo amekuwa anazichezea.
Kile ambacho anajulikana anaweza kukifanya, anatakiwa akifanye kwa kiwango na ubora wa hali ya juu zaidi na kile kinachoaminika ni udhaifu wake basi anapaswa kukirekebisha ili kisimuathiri.
Ni fursa nyingine kwa Sowah kusafisha jina lake hapa nchini baada ya taswira isiyovutia ambayo baadhi wamemjengea kuanzia alipokuwa akiitumikia Singida Black Stars hadi alipotua Simba na sasa amerudi Singida.