Simba SC

VIWANJA UGENINI KAA LA MOTO LIGI KUU BARA

Vardo May 30, 2026 9:49 am

WAKATI Yanga na Azam zikitibuliwa rekodi kwa kupoteza mechi za kwanza Ligi Kuu Bara, viwanja vya ugenini msimu huu vimeonekana kuwa kaa la moto, huku makocha wakijipanga upya kumaliza kibabe mechi za lala salama.

Hadi sasa imebaki mizunguko mitano kumaliza Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026 ambapo Yanga ndio inaongoza kwa pointi 60, Simba ikifuata kwa pointi 58, huku Azam ikiwa ya tatu na pointi 52.

Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwa pointi 41. KMC inaburuza mkia kwa pointi tisa.

Hata hivyo, wakati ligi ikielekea ukingoni viwanja vya ugenini vimeonekana kuwa mwiba mchungu kwa timu za Ligi Kuu, ambapo zipo baadhi yake hazijaonja ushindi ikiwa ni aidha sare au kuchezea vipigo.

Utamu zaidi pia katika viwanja hivyo ni ukame wa mabao ikilinganishwa na msimu uliopita iliposhuhudiwa baadhi ya timu zikishinda kwa idadi kubwa ya mabao na wachezaji kung’ara.

Mwanaspoti imeangalia baadhi ya timu zilizokutana na ugumu kwenye viwanja hivyo huku makocha na wahezaji wakieleza utofauti wa nyumbani na ugenini katika mashindano hayo msimu huu.

MTIBWA SUGAR

Pamoja na kurejea Ligi Kuu msimu huu, Mtibwa Sugar haijawa na matokeo mazuri kwa ujumla katika mechi zake na presha kwa timu hiyo si ndogo katika kukwepa kushuka daraja.

Mtibwa Sugar iliyowahi kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo mwaka 1999 na 2000, ipo nafasi ya 12 kwa pointi 27 ambapo ikizubaa inaweza kufikiwa na timu yoyote iliyopo chini yao.

Wakati ‘Wakata miwa’ hao wakipiga hesabu za kubaki salama Ligi Kuu, ni miongoni mwa timu ambazo hazijaonja ushindi wowote ugenini hadi sasa huku ikiwa ni sare na kuchezea vichapo tu.

Katika michezo 11 iliyocheza ugenini imepoteza sita dhidi ya Singida BS 4-0, Fountain Gate 2-1, Azam 3-0, Yanga 2-0, Mashujaa 1-0 na TRA United 2-1, huku sare zikiwa tano mbele ya Simba 1-1, JKT Tanzania 0-0, KMC 0-0, Dodoma Jiji 0-0 na Coastal Union 1-1. Ugenini imefunga mabao manne pekee, ikiruhusu 16. Imekusanya pointi tano.

KMC

Vibonde hao wa Ligi Kuu waliobakiza dakika 90 tu kujua hatma yao kushuka au kucheza play off, rekodi yao katika mechi za ugenini zimeonekana kuwa ngumu kwa kutopata ushindi wowote.

Timu hiyo iliyowahi kutesa Ligi Kuu na kuwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019-2020, imecheza mechi 13 ugenini ambapo imepoteza 12 na sare moja dhidi ya Coastal Union iliyoisha kwa 1-1.

Mechi ilizopoteza ni dhidi ya Azam 3-0, Mtibwa 4-3, Singida BS 1-0, JKT Tanzania 1-0, Mbeya City 3-2, Dodoma Jiji 2-1, Namungo 1-0, TRA United 3-0, Pamba Jiji 3-0, Yanga 4-1 na Prisons 1-0. Ipo nafasi ya 16 kwa pointi tisa.

Katika michezo hiyo imefunga mabao nane na kuruhusu 28 ikijiweka katika mtihani mzito wa kukwepa aibu ya kushuka daraja huku ikisubiri muujiza katika michezo mitano iliyobaki.

Kwa sasa timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, mchezo ujao dhidi ya TRA United, Juni 12, 2026 ikipoteza shughuli itaishia hapo. Katika mechi 13 za ugenini,

TANZANIA PRISONS

Maafande hao ambao wanaomba huruma kwa sasa kutokana na matokeo waliyonayo, hali haipo nyumbani tu kwani hata ugenini mambo yamewawia vigumu kwa kukosa ushindi.

Katika michezo 12 iliyocheza ugenini imeshinda miwili dhidi Mbeya City 2-1 na Pamba Jiji 3-2 huku ikipoteza mechi tisa, sare moja na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi 20, matokeo ambayo si mazuri kwao.

Timu hiyo imefunga mabao saba na kuruhusu 20.

FOUNTAIN GATE

Timu hii ambayo inapambania kutoshuka daraja, imecheza mechi 14 za ugenini hadi sasa, ambapo ime shinda tatu, sare nne ikipoteza saba huku ikiruhusu wavu wao kuguswa mara 20, yenyewe imefunga mabao 10. Pointi ilizokusanya ni 13.

Kwa jumla, timu hiyo iliyohamishia mechi zake za nyumbani jijini Arusha, inakamata nafasi ya tisa kwa pointi 29.

MBEYA CITY

Timu hii iliyorejea Ligi Kuu msimu huu licha ya kusuasua kwa matokeo ya jumla, lakini imekutana na ugumu wa viwanja si nyumbani Sokoine au ugenini kwani mwenendo wake haujawa imara.

Katika mechi za nyumbani imeshinda mbili tu dhidi ya Tanzania Prisons mabao 2-1 na KMC mabao 3-2 ilipotumia uwanja wa Tanzanite Kwaraa mjini Babati kama uwanja wa nyumbani.

City ni miongoni mwa timu mbili vinara iliyokosa pointi tatu katika mechi za nyumbani huku ikishinda michezo minne tu ugenini na sare moja ikikusanya pointi 13, imepoteza nane, ikifunga mabao 11 na kuruhsu 23.

YANGA, AZAM HOI

Ukitaja walioumizwa na viwanja vya ugenini ni pamoja na bingwa mtetezi Yanga na Azam waliojikuta wakidondosha pointi tatu kwa mara kwenye Ligi Kuu.

Azam ndiye alianza kuonja machungu huko jijini Arusha alipoingia kwenye anga za TRA United na kulazwa mabao 4-1 ikiwa ni mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kufungwa bingwa huyo wa msimu wa 2013-2014.

Yanga nao walijikuta wakichapika dhidi ya Dodoma Jiji, mchezo uliopigwa uwanja wa Airtel mkoani Singida, walipozabwa mabao 3-2 ikiwa ni kipigo cha kwanza kwao msimu huu.

Miamba hiyo kabla ya kupoteza michezo hiyo zilikuwa hazijapoteza mchezo wowote kwenye ligi na mashindano mengine ya ndani na kujikuta wakitibuliwa rekodi zao.

Timu nyingine zinazosota na matokeo ya viwanja vya ugenini ni Coastal Union iliyoshinda mechi mbili sawa na Dodoma Jiji, Namungo na Mashujaa zimeshinda moja.

Simba ndiyo timu pekee haijapoteza ugenini ikishinda nane na sare tano.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amesema ikiwa ni muda mfupi tangu akabidhiwe timu hiyo, ushindi wa mechi moja ugenini kwake si matokeo mabaya ikizingatiwa ugumu wa ligi.

“Nimepata ushindi mmoja ugenini lazima nishukuru kwa sababu kila timu imejipanga ukizingatia na dakika hizi za lala salama, tunaendelea kujipanga na michezo iliyobaki kusaka pointi tatu bila kujali tunacheza wapi,”  anasema Elias.

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shedrack Nsajigwa amesema ratiba ya michezo watakayocheza, hakuna hesabu zozote zaidi ya pointi tatu.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema matokeo yao ya jumla yamekuwa magumu kutokana na kutokuwa na uwanja maalumu wa nyumbani, akitoa matumaini kwa mashabiki.

“Ni kweli hatujashinda ugenini, lakini mbali na hivyo tumekuwa na matokeo si mazuri sana kwakuwa tulifungiwa uwanja wa Jamhuri Morogoro, lakini tunahitaji pointi tisa kati ya 21 zilizobaki ili tuwe salama,”  anasema Kifaru.

SEIF KARIHE AFICHUA JAMBO MASHUJAA TEGISI ATAMANI KUCHEZA NA FEI TOTO AZAM FC