Michezo Bongo

SEIF KARIHE AFICHUA JAMBO MASHUJAA

Vardo May 30, 2026 9:43 am

NYOTA wa Mashujaa, Seif Karihe amekiri kukutana na ugumu wa ligi msimu huu akitoa matumaini kwa mechi tano zilizobaki kufufuka, huku akisisitiza timu hiyo kutoshuka daraja.

Karihe aliyewahi kutesa na timu kadhaa za Ligi Kuu akizitumikia kwa mafanikio ikiwamo Lipuli, Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar akiwa kinara wa mabao kwa timu hizo, msimu huu mambo yameonekana kutomwendea sawa.

Katika michezo 25 ilizocheza Mashujaa hadi sasa, straika huyo amecheza mechi mbili za ligi na mmoja wa Kombe la Shirikisho la CRDB, ambapo hajafunga bao wala kuasisti.

Mashujaa ikikamata nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 26. Nyota huyo mara ya mwisho akiwa Mtibwa Sugar alikuwa mfungaji bora kikosini akitupia mabao tisa, huku misimu mitatu Dodoma Jiji akifanya hivyo na hadi anaondoka alifunga mabao nane.

Karihe amesema msimu huu umekuwa mgumu kwake kwani hata mwanzo wa ligi alikumbwa na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda na aliporejea amekutana na ushindani wa namba.

Amesema suala lingine ni kutokana na mahitaji ya benchi la ufundi kuwa na mahitaji yao kulingana na mechi husika, akieleza kuwa michezo mitano iliyobaki huenda ikamrejesha na akafanya kweli.

“Kikubwa tunaangalia matokeo ya timu kwa ujumla, lakini kuheshimu mipango ya kocha, bado naamini nikipata nafasi naweza kufanya vizuri kwakuwa mechi tano si ndogo kwa mchezaji mwenye uwezo, nia na uzoefu wa kusaidia timu,” amesema Karihe.

 Ameongezakuwa kwa muda huu wakati ligi imesimama wakiwa mapumziko mafupi, ataendelea kujifua mwenyewe ili anaporudi mazoezini awe fiti kwa michezo ya lala salama.

“Matarajio yetu timu haishuki kwakuwa wachezaji tunao uwezo na kila mmoja ana ari, nguvu na matamanio ya kufanya vizuri, kikubwa ni ushirikiano na kujituma kwa wachezaji,” amesema straika huyo.

PAMBA JIJI YAZOA BEKI NAMUNGO VIWANJA UGENINI KAA LA MOTO LIGI KUU BARA