ULE UTAMU WA CHAMPIONSHIP SASA UMEFIKIA PAZURI
UHONDO wa Ligi ya Championship umefikia hatua nzuri kwa sasa, ambapo leo Jumamosi itashuhudiwa mechi zote nane zikipigwa za raundi ya 27, huku ushindani ukiongezeka kwa timu zinazopigania kupanda Ligi Kuu na zinazopambana kutoshuka daraja.
Vinara wa Ligi hiyo, Geita Gold yenye pointi 65, ikishinda mechi 20, sare tano na kupoteza moja, baada ya kutoka suluhu (0-0), mechi ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar, itakuwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya, Mbeya kucheza na KenGold.
KenGold inayoshika nafasi ya nane na pointi 33, baada ya kushinda mechi tisa, sare sita na kupoteza 11, inaingia kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya jijini, Mbeya, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Songea United mabao 2-1.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu, baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Hata hivyo, KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu Bara na kushuka daraja msimu wa 2024-2025, ikimaliza mkiani na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar, iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
Kwa upande wa Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, ikiwa na aliyekuwa Kocha, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Geita ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Timu hiyo inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila aliyejiunga nayo akitokea Bigman FC, anaipambania kuirejesha Ligi Kuu Bara kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kuzifundisha pia, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mtibwa Sugar.
Kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo mji wa Songea Mkoa wa Ruvuma, Songea United inayoshika nafasi ya 12 na pointi 29, baada ya kuchapwa na KenGold mabao 2-1, itaikaribisha Kagera Sugar iliyotoka suluhu (0-0) mechi ya mwisho dhidi ya Geita Gold.
Kagera iliyo nafasi ya pili na pointi 62, baada ya kudumu katika Ligi Kuu kwa miaka 20, tangu iliposhiriki mwaka 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, ikishinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15 na pointi 23.
Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
Stand United ‘Chama la Wana’, baada ya kuchapwa mechi ya mwisho mabao 3-1, dhidi ya Gunners FC, inarejea nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga kuikaribisha Bigman FC, iliyotoka kushinda bao 1-0, ugenini mbele ya Hausung FC.
Msimu wa 2024-2025, Stand ilimaliza nafasi ya tatu na pointi 61, ambapo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara, ikianza kwa kuiondosha Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, katika Ligi ya Championship kwa jumla ya mabao 4-2. Baada ya Stand kuitoa Geita Gold, ikacheza ‘Play-Off’ nyingine na Fountain Gate iliyotolewa pia hatua hiyo na maafande wa Tanzania Prisons kwa jumla ya mabao 4-2, ambapo kikosi hicho kilikwama kupanda baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-1.
Kwa upande wa Fountain, ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29 katika Ligi Kuu msimu wa 2024-2025 na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza ya 13 na pointi 31, kwenye mechi ya mtoano na kikosi hicho cha maafande kushinda jumla ya mabao 4-2.
Stand United inayoshika nafasi ya 13 na pointi 24, ilishuka daraja msimu wa 2018-2019, ikimaliza nafasi ya 19 na pointi 44, baada ya kikosi hicho kushinda mechi 12, kikitoka sare nane na kupoteza 18, huku kikifunga mabao 38 na kuruhusu 50.
Kwenye Uwanja wa Amani uliopo mjini Njombe, Hausung FC inayoburuza mkiani mwa msimamo mwa nafasi ya 16 na pointi nane, baada ya kuchapwa bao 1-0, dhidi ya B19 FC, itaikaribisha Barberian FC iliyochapwa pia 1-0 na maafande wa Transit Camp.
Baada ya Mbuni FC kuchapwa na ndugu zao wa TMA FC bao 1-0, katika mechi iliyopita ya ‘Derby ya Monduli’, itabaki kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini, Arusha kucheza dhidi ya African Sports ya Tanga iliyochapwa na Polisi Tanzania 3-1.
Mbeya Kwanza iliyoichapa Bigman FC mabao 2-1, itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini, Tabora kucheza dhidi ya Gunners FC ya jijini, Dodoma yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuichapa Stand United ‘Chama la Wana’ mechi ya mwisho 3-1.
Timu hiyo iliyouzwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu wa 2024-2025, ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu kwenda Championship msimu wa 2021-2022, baada ya kumaliza mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi 25. Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.
Kwenye Uwanja wa Kituo cha TFF Kigamboni, jijini, Dar es Salaam, wenyeji B19 FC itawakaribisha maafande wa Transit Camp, huku Polisi Tanzania inayopigania kupanda Ligi Kuu ikiwa Uwanja wa Ushirika, mjini, Moshi kuikaribisha TMA FC ya Arusha.