Usajili wa Mutuyimana Sandrine Yanga Princess
Yanga SC

Yanga Princess Kukamilisha Usajili Wa Mutuyimana Sandrine Kutoka Rwanda

Vardo July 19, 2026 7:20 pm

DAR ES SALAAM: Klabu ya Yanga Princess ipo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji hatari raia wa Rwanda, Mutuyimana Sandrine, kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea klabu ya Inyemera WFC ya nchini kwao.

Sandrine anatua Jangwani akiwa na rekodi ya kuvutia, baada ya kuibuka miongoni mwa wafungaji bora kwenye Ligi Kuu ya Wanawake nchini Rwanda. Nyota huyo alifunga mabao 10 na kuongoza chati ya ufungaji, huku pia akiwa ni tegemeo kubwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Rwanda (She Amavubi).

Kabla ya kufikia makubaliano ya mkataba huo, Sandrine amekuwa nchini Tanzania kwa zaidi ya mwezi mmoja akifanya majaribio na mazoezi na Yanga Princess. Benchi la ufundi la timu hiyo lilikuwa likipima uwezo wake kabla ya kujiridhisha na kumpatia rasmi dili hilo la miaka mitatu.

Inaelezwa kuwa katika kipindi chote cha majaribio, Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema ‘Mourinho’, alivutiwa mno na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu alioonyesha mshambuliaji huyo.

Mutuyimana anasajiliwa na Yanga Princess ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mnyarwanda mwenzake, Jeannine Mukandayisenga, ambaye hivi karibuni aliuzwa kwenda klabu ya Wuhan Jiangda WFC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini China.

Fainali Ya Argentina vs Spain: Vita Ya Messi Na Yamal Kulikabili Kasino? Rasmi: Simba SC Yashusha Kiungo Mashine Kutoka Pamba Jiji FC!