Ujenzi Uwanja Wa Fumba Zanzibar Wafikia Asilimia 65: Maandalizi Ya AFCON 2027
ZANZIBAR: Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imethibitisha kuwa ujenzi wa mradi mkubwa wa Uwanja wa Michezo wa Zanzibar (Fumba Stadium) unakwenda kwa kasi ya kuridhisha, huku ukiwa tayari umekamilika kwa asilimia 65 na hakuna hatua yoyote iliyosimama.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, wakati wa ziara yake maalum ya kukagua maendeleo ya miundombinu inayojiandaa kwa mashindano ya AFCON 2027. Mbali na Fumba, Waziri Riziki alikagua pia viwanja vya Matemwe na Matumbaku.
Katika ziara hiyo, Waziri Riziki alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa. Aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi huku wakizingatia viwango vya ubora vya kimataifa vinavyotakiwa na mashirikisho ya soka.
Pongezi kwa Rais Mwinyi na Fursa kwa Wananchi
Waziri Riziki alimpongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada na hatua kubwa anazochukua kuimarisha sekta ya michezo kupitia miundombinu ya kisasa. Aliwaasa wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili inufaishe vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia, aliwahimiza wananchi kuchamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na mashindano ya AFCON 2027, zikiwemo sekta za ujasiriamali, utalii, na biashara za huduma kwa wageni watakaomiminika nchini.
Viwango vya CAF na FIFA Kuzingatiwa
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi wa mradi huo kutoka kampuni ya Orkum Group, Simbo Nkya, alihakikisha kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika kwa wakati na unakidhi vigezo vyote vikali vilivyowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).