MATAJI SABA NYOTA WA SIMBA QUEENS WAWEKA REKODI TANZANIA
MENEJA wa Idara ya Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameendelea kujivunia mafanikio yanayoandikwa na timu ya wanawake ya Simba Queens, ambayo imeendelea kutawala soka la wanawake nchini kwa kuweka rekodi mbalimbali za kihistoria.
Licha ya kukosolewa na baadhi ya wapinzani wake kwamba tangu ajiunge na Simba hajafanikiwa kushuhudia timu ya wanaume ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ahmed ameendelea kupata faraja kupitia mafanikio makubwa ya Simba Queens.
Timu hiyo imeendelea kuonyesha ubabe wake katika soka la wanawake Tanzania, huku ikizidi kuandika historia na kujijengea heshima ndani na nje ya nchi. Tofauti na Simba Queens, wapinzani wao wa jadi Yanga Princess bado hawajawahi kutwaa ubingwa wa ligi tangu waanze kushiriki mashindano hayo.
Mbali na mafanikio ya timu kwa ujumla, Simba Queens pia imeweka rekodi kupitia baadhi ya nyota wake walioingia kwenye orodha ya wachezaji wenye mataji mengi zaidi katika soka la wanawake nchini. Wachezaji hao ni Janeth Shija, Doto Evarist na Fatuma Issa.
Kila mmoja wa nyota hao sasa anamiliki mataji saba akiwa na Simba Queens, yakiwemo mataji matano ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL), taji moja la CECAFA Club Championship na moja la Community Shield, jambo linalowafanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanikiwa zaidi katika historia ya mchezo huo nchini.
Akizungumzia mafanikio hayo, Ahmed ameonyesha fahari kubwa kwa kile ambacho Simba Queens wamekifanya, akiwataja Janeth, Doto na Fatuma kama miongoni mwa wanawake waliofanikiwa zaidi katika soka la Tanzania kutokana na mchango wao mkubwa ndani ya klabu hiyo.
Ahmed amesisitiza kuwa mafanikio ya Simba Queens hayaishii kwenye mataji ya ndani pekee, bali pia timu hiyo imefanikiwa kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, hatua inayoonyesha ukuaji wake na ushindani wake katika ngazi ya kimataifa.
Kwa sasa Simba Queens inaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika soka la wanawake nchini, huku mashabiki wake wakiamini kuwa kikosi hicho kina uwezo wa kuendelea kuvunja rekodi zaidi na kufikia malengo makubwa zaidi, ikiwemo kuongeza idadi ya mataji ya ligi katika miaka ijayo.