Yanga SC

PACOME AKIWA FITI, YANGA YAONGEZA KASI YA UWINDAJI WA MAKOMBE

Vardo June 4, 2026 1:28 pm

YANGA imepata habari njema kuelekea hatua za mwisho za msimu baada ya kiungo mshambuliaji wake tegemeo, Pacôme Zouzoua, kurejea mazoezini akiwa fiti na tayari kusaidia timu katika harakati za kusaka mataji.

Nyota huyo raia wa Ivory Coast alikuwa nje ya uwanja kwa kipindi kadhaa kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mchezo dhidi ya Singida Black Stars, hali iliyomlazimu kukosa mechi kadhaa muhimu za timu hiyo.

Kutokana na majeraha hayo, Pacôme alilazimika kuendelea na matibabu na programu maalumu ya kurejea kwenye kiwango chake, huku benchi la ufundi likisubiri kwa hamu kurejea kwake.

Sasa kiungo huyo amerejea rasmi mazoezini na kuungana na wachezaji wenzake katika maandalizi ya mechi zilizobaki msimu huu, jambo ambalo limeongeza chachu ndani ya kikosi cha Wananchi.

Kurejea kwake kumempa ahueni kubwa kocha Abdihalim Moalin ambaye anaamini uzoefu na ubora wa mchezaji huyo vitakuwa muhimu katika kipindi hiki cha mwisho cha msimu.

Yanga bado ina kazi ya kupigania mataji mawili makubwa, likiwemo la Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB, ambapo timu hiyo imebakiwa na michezo saba muhimu ya kuamua hatma ya msimu wao.

 

Kwa sasa Pacôme na wenzake wanaendelea kujifua kwa nguvu wakijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC utakaochezwa Juni 13, 2026 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, huku mashabiki wa Yanga wakitarajia kumuona nyota huyo akirejea uwanjani kwa kiwango chake bora.

MATAJI SABA NYOTA WA SIMBA QUEENS WAWEKA REKODI TANZANIA HAKUNA KISINGIZIO YANGA WOTE WAPO VITANI